……………………………………………………………….
Na.Mwandishi Wetu.
Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhandisi Joseph Nyamhanga ameutaka Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Jijini Dar es Salaam DART, kuandaa mapema utaratibu wa kumpata mtoa huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka katika Barabara ya Kilwa ambao ujenzi wa miundombinu awamu ya pili munaendelea.
Mhandisi Nyamhanga alisema kuwa ili kuwezesha kuanza huduma ya Mabasi na mtoa huduma kamili,inabidi kuanza hatua za manunuzi mapema kabla ya ujenzi wa miundombinu ya awamu ya pili kukamilika
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa kituo kikuu cha Mabasi Yaendayo Haraka kilichoko Mbagala Jijini Dar es Salaam, Mhandisi Nyamhanga amesema maandalizi ya mtoa huduma yakikamilika mapema yataepusha ulazima wa kuanza huduma ya Mabasi katika kipindi cha mpito.
“Mtendaji Mkuu nakuagiza wewe na timu yako mkae muone namna mtakavyotafuta mtoa huduma ya Mabasi katika barabara hii ya Kilwa ili tatizo la kukamilika kwa miundombinu bila kuwa na mtoa huduma lisijitokeze tena kama ilivyokuwa kwa awamu ya kwanza ya mradi unaoanzia Kimara hadi Kivukoni, Moroco na Gerezani ambapo miundombinu ilikamilika lakini hakukuwa na mtoa huduma” Alisema Mhandisi Nyamhanga.
Alisema wakazi wa Mbagala na maeneo ya jirani wawe tayari kutumia fursa ya usafiri wa DART kwa vile Serikali iko katika hatua mbalimbali za kujenga miundombinu ya barabara za DART ambapo kukamilika kwa ujenzi huo kunaweza kupunguza msongamano kwa kiasi kikubwa.
Aidha amesema kuwa miradi yote mikubwa ya kimkakati inalenga kuwaondolea kero Watanzania na kuinua uchumi wan chi pamoja na na kipato cha mwananchi mmoja mmoja hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania imepiga hatua kimaendeleo kwa kuingia katika nchi za uchumi wa kati.
Akizungumzia maendeleo ya ujenzi wa kituo Kikuu cha Mbagala ambao pia unahusisha ujenzi wa karakana, Mhandisi Barakael Mmari amesema ujenzi huo umefikia asilimia 52.
Alisema Kituo hicho Kikuu kinauwezo wa kuegesha Mabasi Zaidi ya 400 na kitakuwa na majengo ya huduma mbalimbali za kijamii.
Amesema usanifu na ujenzi wa eneo hilo umebadilisha uelekeo wa maji ambayo yalikuwa yaelekee kwenye makazi ya watu badala yake sasa yataelekezwa barabarani kwenye mfereji mkubwa ambao utayapeleka mtoni na hivyo kuepuka madhara ya kimazingira.
Akifafanua mpango wa kuanza kutoa huduma ya Mabasi, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mabasi Yaendayo Haraka Mhandisi Ronald Lwakatare, amesema mara ujenzi wa miundombinu inayohusisha barabara, vituo mlisho, kituo Kikuu pamoja na Karakana ukikamilika watakua tayari kutoa huduma ya Mabasi.yako vizuri na wanajipanga kutoa huduma mara tu mradi utakapokamilika.
Amesema maagizo ya Katibu Mkuu ameyachukua na atakaa na timu yake kuona namna bora ya kuyatekeleza ili azma ya kuwapelekea huduma ya Mabasi Yaendayo Haraka wakazi wa Mbagala itimie.
Ziara ya Katibu Mkuu TAMISEMI ilikua ni mahsusi kwa ajili ya kukagua shughuli za maendeleo zinazotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Dkt.John Pombe Magufuli, katika mkoa wa Dar es Salaam ikihusisha Wilaya zote tano.