**********************************
Na John Walter-Manyara
Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Manyara (MNRPC) kwa kushirikiana na Umoja wa Klabu za waandishi wa habari Tanzania (UTPC) wameendesha mafunzo ya siku moja kwa waandishi wa habari ambao ni wanachama wa klabu hiyo juu ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo COVID-19 na namna ya kujilinda, kufanya kazi na kujikinga kwenye magonjwa hayo.
Mafunzo hayo yamefanyika leo Agosti 15, 2020 katika ukumbi wa Giraffe katika hotel ya White rose mjini Babati yakiwezeshwa na wataalam wa afya kutoka ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoani humo.
Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa wilaya ya Babati Lazaro Twange ametoa wito kwa waandishi wa habari kuzingatia weledi katika Kazi zao pindi wanaporipoti matukio ya magonjwa ya mlipuko ili kuondoa taharuki kwa wananchi.
Amesema mafunzo hayo yaliyotolewa yanagusa sehemu kubwa ya jamii na njia zake za uenezaji ni rahisi kuzuilika kupitia elimu itakayotolewa kupitia vyombo vya habari.