………………………………………………………………………….
ADELADIUS MAKWEGA – WHUSM, Dodoma.
Serikali imesema haijatoa vitisho vyovyote kwa vyombo vya habari nchini kuhusu kuchapishwa au kuzuia machapisho ya habari za uchaguzi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Kauli hiyo imetolewa leo Agosti 13, 2020 asubuhi katika Kipindi cha Tuongee Asubuhi cha Televisheni ya Startv na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Dkt.Hassan Abbasi akiwa katika studio za televisheni hiyo Jijini Dodoma.
“Mifumo ya taasisi kama vile TCRA na Idara ya habari – MAELEZO kwa kuongozwa na Sheria na Kanuni zake zimewekwa ilikufanikisha kazi au taaluma ya Mwanahabari iweze kufanyika vizuri,” alisema Dkt. Abbasi.
Akiendelea kuzungumza katika mahojiano ya kipindi hicho Dkt.Abbasi alisema serikali imeweka mazingira mazuri kwa mwanahabari yoyote kufanya kazi yake vizuri, bila kumuumiza mtu mwingine, kinyume chake basi Sheria na Kanuni hizo zitafanya kazi yake.
“Sheria ya Huduma za Habari ya Mwaka 2016 siyo rungu la kuponda taaluma ya habari bali ni kama grisi ya kumfanya mwanahabari kufanya kazi yake kwa weledi na kuifanya taaluma hii iheshimike kama taaluma nyingine”, aliongeza Dkt.Abbasi.
Kwa upande wa vyombo vya habari vya Kimataifa Dk.Abbasi alieleza kuwa Serikali imeweka kanuni za uendeshaji wa vyombo vya habari vinavyorusha matangazo hapa nchini, hivyo jambo hilo linapaswa kufahamika na kila mmoja wetu pia ni jambo zuri kujadiliwa kwa kina ili pawepo na ufahamu wa kanuni hizo, Kwani hatua zitapochukuliwa pasionekane pana uonevu kwa chombo chochote cha kimataifa.
Aidha, Dkt.Abbasi alifafanua kuwa Matangazo kutoka nje yana mchango kwa taifa letu tangu enzi, hivyo matangazo hayo yataendelea kupokelewa na kurushwa kama kawaida ila wanapaswa kuomba leseni ili wanaporusha matangazo hayo kwa chombo cha ndani au cha nje waweze kunawajibika na maudhui hayo.
Mjadala huo uliyodumu kwa zaidi ya saa moja na nusu ulibebwa na mada inayosema “Uhuru wa vyombo vya habari kuelekea uchaguzi mkuu wa 2020 huku kwa upande mwingine kukiwa na madai kuwa kumekuwa na changamoto juu ya vyombo vya habari vinavyoripoti habari za uchaguzi.
************Mwisho**********