*************************
Shirika la Red Cross limetoa msaada wa zaidi ya Sh milioni 34 na huduma za kibinadamu ikiwamo magodoro kwa kaya 459 katika kata za Kigogo na Tandale Dar es Salaam zenye watu 2,327 zilizoathiriwa na mafuriko hivi karibuni
Akizungumza Dar es Salaam leo Mkurugenzi wa Idara ya Maafa ya shirika hilo, Renatus Mkaruka, alisema shirika hilo limeanzisha utaratibu wa kutoa fedha kwa waathirika wa maafa ambao haukuwapo awali ili kuwawezesha kumudu gharama nyingine za maisha ambazo haziwezi kubainiwa na shirika hilo.
Aidha Bw.Mkaruka amesema tangu kuanzishwa kwa shirika hilo mwaka 1962, limekuwa likitoa mahitaji ya kibinadamu ikiwamo magodoro na mablanketi lakini sasa wameamua kuliangalia kwa jicho la ubunifu zaidi kwa kuanza kutoa fedha taslimu.
Pamoja na hayo Bw. Mkaruka ameongeza kuwa walionufaika na msaada huo ni wale walioathirika na mafuriko yaliyosababishwa na mvua zilizonyesha Aprili na Mei mwaka huu jijini humo.
“Lakini pamoja na kutoa misaada hiyo ya kibinadamu gharama ya kuifikisha kwa walengwa vitu hivyo ni kubwa kwa sababu klaribu robo ya gharama huishia kwenye usafiri wa kupeleka vitu hivyo kwa waathirika wa maafa.Mfano unasaidia watu 2,000 ni vigumu kupata mawazo ya kila mmoja ila badala yake tunatoa misaada hiyo kwa jumla kwa kuhisi kuwa kwa kuwa wamepatwa na mafuriko wanaweza wakawa hawana magodoro mablanketi na vitu vingine muhimu,” Amesema Bw.Mkaruka.
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Menejimenti ya Maafa Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw.Bashiru Taratibu, amesema utaratibu huo wa utoaji fedha tayari umekuwa ukitumika katika baadhi ya nchini ikiwamo Kenya na kuonesha mafakio makubwa.
“Nchini nyingi zilikuwa zikitoa mahitaji muhimu lakini kwa miaka ya karibuni wameanza kutoa fedha na jirani zetu Kenya wameanza kufanya hivyo kwa muda kiasi. Gharama za kutoa fedha ni ndogo kuliko kubeba vitu kuwapelekea watu walioathiriwa na maafa” amesema Bw.Taratibu.