***********************************
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
Agost 3
WAKAZI wa Kitongoji cha Kisabi ,kata ya Mtongani Kibaha vijijini Mkoani Pwani, wanataka Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi William Lukuvi, awasaidie kuondokana na manyanyaso wanayoyapata ya kutakiwa kuondoka eneo hilo ambalo waliishi kutokana na kulikuta pori.
Licha ya eneo hilo kudaiwa kuwa mali ya taasisi hiyo, lakini ndani yake vimepimwa viwanja vinauzwa kati ya sh. 300,000 hadi milioni moja, huku wakitakiwa na wao wavinunue la sivyo wasitegemee kuishi hapo.
Wakitoa kilio hicho ,wameeleza wanaishi eneo hilo kwa hofu kubwa, wakitishiwa watabomolewa nyumba zao wakidaiwa hapo ni mali ya Taasisi ya DIMALA iliyokuwa inajihusisha na ufugaji.
Wakazi Fatima Ramadhani, Hassani Nzolelanga, Kassimu Bakari, Asia Ngoengo na Hamisi Abdallah, walisema kuwa mwaka 2014 walikuwa wanaishi ng’ambo ya mto Ruvu, wakakumbwa na mafuriko wakaamua kuingia eneo hilo na kuweka makazi .
“Tuliona hapa kuna msitu mkubwa, tukasafisha kutokana na msitu mkubwa paliitwa machinjioni, waharifu walifanya mauaji na ubakaji”
Chakushangaza wanaambiwa wamevamia wakati hata mwenyekiti wa Kitongoji wamemchagua wakiwa mahala hapo.
Zolelanga alieleza, hadi sasa wanajishughulisha na kilimo ambapo kipato chao wanakitumia kuendesha shughuli za kifamilia ikiwemo kusomesha watoto na nyingine nyingi.
“Tumeishi kwa miaka sita, serikali inatutambua, lakini tunasikitishwa na kauli kutoka kwa viongozi wetu kutuambia tunatakiwa tuondoke, wakidai ni eneo la DIMALA, tunahoji mbona halikuendelezwa badala yake kulikuwa na msitu mkubwa?,” alihoji Zolelanga.
Nae Mwenyekiti wa Kitongoji hicho Yahaya Mzee alisema, amewazuia kujenga nyumba za kudumu kutokana na eneo hilo kuwa la Kampuni ya DIMALA, iliyokuwa inajihusha na ufugaji wa ng’ombe, na wajiorodheshe ili afikishe ombi kwa meneja kama wataweza kuwapatia eneo.
“Walileta orodha yao ya watu si zaidi ya 45, wakati wao wapo zaidi ya 100 nikawaambia warudi wawaandike na wenzao wote, ili itakapowafikia walengwa kama watawapatia eneo wajue wapo wangapi na ukubwa gani wa ardhi ambayo wataitoa” alieleza Yahaya.