Vitambulisho vya Wajasiliamali Wadogo vilivyotolewa na Rais wa Tanzania Dkt. John Magufuli vimepokelewa vyema na Wajasiliamali hao ambao wamemshukuru Rais Magufuli kwa kuwakomboa kiuchumi kwani hawasumbuliwi tena.
Hayo yamejitokeza kwenye ziara ya ghafla aliyoifanya Afisa Tarafa Mihambwe Emmanuel Shilatu alipotembelea Wajasiliamali Wadogo kwenye gulio kwa lengo la kukagua vitambulisho ambapo alikuta asilimia kubwa wanavyo jambo linalotoa picha ya kubaliko la vitambulisho hivyo.
Gavana Shilatu alifanya ziara ya kukagua vitambulisho hivyo kwenye gulio lililofanyika kijiji cha Mwenge A kata ya Kitama ambapo aliwapongeza Wajasiliamali hao kumwitika vyema Rais Magufuli.
“Nimepita nikikagua vitambulisho nimekuta asilimia 95 ya Wafanyabiashara wanavyo na wachache walikuwa wamevisahau na wengine walikuwa wamevipoteza na wameshatoa taarifa Polisi ya kupotea huko. Nawapongeza Wajasiliamali wote kwa kuendana na kasi ya Rais Magufuli ya kulipa kodi na kufanya kazi.” Alisema Gavana Shilatu
Wakati wa ukaguzi huo, Wajasiliamali hao walisema vitambulisho hivyo ni kinga ya manyanyaso yao na tiba ya ukuaji kiuchumi hivyo wana kila sababu ya kuvinunua kwa maslahi mapana kwao na kwa Taifa.
“Mwanzo tuliona kama manyanyaso ila sasa tunavigombea kwani tumeona umuhimu wake ndio maana wengi sana tunavyo. Tunamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujalia Dkt. Magufuli, Rais mwenye maono kwa Watu na Taifa lake.” Alisikika akisema mmoja wa Wajasiliamali hao wadogo.
Vitambulisho vya Wajasiliamali Wadogo vimetolewa na Rais Magufuli ambavyo vinauzwa kwa Tsh. Elfu ishirini tu, vimeonyesha msaada mkubwa kwa Wajasiliamali Wadogo kwani hawasumbuliwi tena na kero ya ushuru na sasa vinawasaidia kukuza uchumi wao.