………………………………………………………………………………..
NA MWAMVUA MWINYI,PWANI
WAKAZI wapatao 5,700 katika vitongoji Tisa ,Kijiji cha Buyuni kata ya Vigwaza ,Chalinze, Pwani wanatarajia kuondokana na kero ya kutumia maji ya bwaloni yasiyo salama kiafya ,baada ya kupokea kisima cha maji safi ,kinachohifadhi maji lita 10,000 ,kutoka kwa shirika la WHO IS HUSSAN .
Shirika hilo linalojishughulisha kusaidia jamii ,limemkabidhi kisima hicho ,kilichogharimu milioni 36 ,diwani anaemaliza muda wake kata ya Vigwaza ,Mohsin Bharwani .
Akikabidhi kisima hicho ,Mwenyekiti wa WHO IS HUSSAIN tawi la Dar -es -salaam Fatma Kermalli alisema ,waliguswa kutoa msaada huo baada ya diwani huyo kuomba hitaji hilo kutokana na wakazi hao kutaabika na kufuata maji umbali mrefu na bwaloni .
“Tulianza ujenzi Februari mwaka huu na kukamilisha ujenzi march mwishoni ,na sasa tumekabidhi kisima baada ya kuona wanakabiliwa na changamoto kubwa ya maji.”:;
Aidha Fatma alibainisha ,wametoa pia misaada kwa wanafunzi 500 na wazazi 200 wa Buyuni shule ya msingi ikiwemo ,mabag,madaftari ,kalamu na kwa wazazi sukari kilo mbili kila mmoja,mchele na kofia.
Pamoja na hilo ,wameahidi kujenga tanki la maji shule ya msingi Buyuni na kuweka solar .
Nae Mohsin Bharwani alieleza ,amekuwa akishirikiana na wadau wa maendeleo kutatua changamoto zinazowakabili wakazi wa Vigwaza ,sanjali na kusaidia makundi maalum milioni 25 ,sadaka na chakula katika kaya maskini milioni 13 na kusaidia miwani kwa wagonjwa wa macho kwa kushirikiana na taasisi ya WHO IS HUSSAIN.
“Mimi ni mwakilishi wa wananchi ,tulikaa tukashaauriana nao na wao walihitaji kusaidia eneo lenye tatizo na kero ya maji na kuona wachimbe kisima hicho kijiji cha Buyuni “
“Si hapa tu lakini wanatarajia kuchimba visima na maeneo mengine ya kata hii “alifafanua Mohsin.
Mohsin aliishukuru shirika la WHO IS HUSSAIN kwa kutoa misaada mbalimbali ya akinamama na watoto ambao ni wanafunzi kwani mabag ,,kalamu ,madaftari ambavyo ni mahitaji muhimu kwa wanafunzi .
Kwa upande wa wakazi wa Buyuni akiwemo Fatuma Omary alielezea ,awali walikuwa wakitumia masaa mawili kufuata maji na kutumia maji ya bwaloni ambayo ni machafu ,ambapo sasa ni neema kwao kupata kisima cha maji.