Katibu Mkuu Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiwa kwenye mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu wa kiwanda cha Pareto cha Mufindi John Power.Katibu Mkuu ameagiza kuwa serikali itapeleka mtaalam wa maabara kufanya kazi kiwandani hapo ili kubaini ukweli juu ya madai ya wakulima kupangiwa bei ndogo ya pareto yao. Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya akiongea na Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda cha Pareto Tanzania Bw.John Power mara alipowasili kiwandani hapo kwa ziara ya kikazi kuhusu utatuzi wa malalamiko ya wakulima kupunjwa bei .Katibu Mkuu Wizara ya KIlimo Bw.Gerald Kusaya ( katikati) akitembelea kiwanda cha Pareto Tanzania kilichopo Mufindi mkoa wa Iringa leo kufuatia malalamiko ya wakulima wa pareto kuwa kiwanda kinatumia maabara inayosababisha wapate bei ndogo.
Serikali imetoa maelekezo kwa kiwanda cha Pareto Tanzania kuhakikisha kinaweka mazingira ya uwazi katika kupima kiwango cha sumu kwenye maua ili wakulima wapate bei nzuri ili kulinda maslahi ya wakulima nchini.
Kauli hii ya serikali Imetolewa leo (11.07.2020 ) wilayani Mufindi na Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya wakati alipofanya ziara ya kukagua na kuongea na menejimenti ya kiwanda cha Pareto Tanzania ( Pyrethrum Company of Tanzania-PCT) kilichopo Mufindi mkoani Iringa.
Kusaya alieleza kuwa serikali inazo taarifa za malalamiko ya wakulima wa zao la pareto kuwa wataalam wanaohusika na kupima viwango vya sumu kwenye maua wanatumia vipimo veye mashaka na kupelekea mkulima kupata bei ndogo za pareto hali inayosababisha wakate tama kuzalisha.
“ Serikali imekuwa ikipokea malalamiko ya wakulima wake wa pareto kuhusu kiwanda hiki cha PCT kutumia vifaa vya maabara ya kupima viwango vya sumu kwenye maua ,jambo hili halikubaliki ndio maana nimekuja hapa Mufindi” alisema Katibu Mkuu Kusaya
Kufuatia hali hiyo Katibu Mkuu huyo wa wizara ya Kilimo alitoa maelekezo sita ambayo kiwanda cha pareto na wadau wengine wanapaswa kuyazingatia ili mkulima apate haki kwa kazi anazozifanya
Kwanza, ni lazima kiwanda kinapotengeneza kigezo cha kupima kiwango cha sumu kwenye maua kujua bei gani itatozwa yaani ‘ K-Factor’ ishirikishe Bodi ya Pareto ,wakulima na mmiliki wa kiwanda ili kuwe na uwazi na kulinda maslahi ya mkulima.
Pili, wizara ya Kilimo itapelekea mtaalam wa maabara ya pareto toka TARI kwa ajili ya kusimamia upimaji wa kiwango cha sumu akiwakilisha serikali muda wote kwa kuangali kazi zinzvyofanyika kwenye maabara ya kiwanda
Tatu, viwanda vyote vya pareto nchini katika kipindi cha miezi sita ijayo havitaruhusiwa kusafirisha nje ya nchi pareto ghafi badala yake vitatakiwa kuweka miundombinu ya kuzalisha bidhaa hapa nchini ili kulinda ajira za watanzania na kuwesaidia zao kuwa na bei nzuri
Agizo la nne la seikali ni kuwa mashamba yote ya uzalishaji mbegu za pareto nchini lazima yasajiliwe na taasisi za utafiti wa Kilimo (TARI) na ile ya udhibiti ubora wa mbegu ( TOSCI).Lengo kuhakikisha wakuima wanapanda mbegu bora na zenye tija kwenye uzalishaji wa pareto nchini.
Kusaya alitaja agizo la tano kuwa halmashauri zote zinazozalisha pareto ziratibu vituo vya ununuzi wa zao hilo na kuwa ni mmarufuku wanunuzi kwenda majumbani kununua pareto kwa wakulima sita halmashauri ziweke utaratibu wa wawekezaji kugawana kanda za uzalishaji pareto na kuingia mikataba na wakulima wa maeneo hayo.
Katibu Mkuu Kusaya alisema agizo la mwisho ni kuwa halmashauri nchini ziratibu na kuhamaasisha wakulima wa pareto kujiunga na vyama vya ushirika ili waweze kupata huduma za ugani kwa karibu na kuwezesha upatikanaji wa masoko.
Kwa upande wake mwaklishi wa kiwanda cha Pareto Tanzania (PCT) Gerald Joseph alisema kiwanda kitaendelea kuhakisha kuwa kodi,tozo na ushuru unaotakiwa kulipwa unalipwakwa mujibu wa sheria na
Aliongeza kusema kuwa watazingatia suala la vipimo na mizani inayotumika kupima pareto ya wakulima inaendelea kuwa sahihi na kuwa wakulima wanapata bei inayostahili .
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Kiwanda Tanzania John Power alisema kiwanda chake kitaendele kuhakikisha kuwa wananunua pareto ya wakulima kwa mujibu wa bei ya soko na kuwa viwango vya ubora lazima vizingatiwe na wakulima wakati wa kuchuma maua ya pareto na kukausha.
Akitoa uzoefu wake kuhusu sekta ya pareto nchini Mkurugenzi wa SAGCOT Center Ltd Dkt Godffrey Kirenga alisema ili mkulima azalishe zao bora la pareto lazima afundishwe vizuri kanuni bora za uzalishaji
Dkt.Kirenga aliongeza kusema “ zao hili ndilo lenye uwezo wa kumpatia mkulima pato la uhakika kwani linalimwa kwa mwaka mzima “ katika maeneo ya mikao ya Iringa,Njombe ,Kilimanjaro ,Manyara na Mbeya
Tanzania ndiye mzalishaji wa pili wa pareto kwa wingi na kupitia kiwanda hiki PCT mwaka 2019 jumla ya tani pareto 2,100 ziliuzwa nje na wakulima walilipwa Dola za kimarekani Milioni 1.539