Afisa Uuguzi wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Mary Haule akiwaelezea wananchi namna ambavyo mashine ya kusaidia kupumua (ventilator) inavyotumika kwa wagonjwa waliolazwa katika chumba cha uangalizi maalum (ICU) wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.Wataalam wa maabara kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakipima vipimo vya damu kwa ajili ya kuangalia magonjwa ya moyo kwa wananchi waliofika katika banda hilo kwa ajili ya kupima afya zao wakati wa Maonesho ya 44 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam.
**********************************
Wananchi waliotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) katika Maonesho ya Sabasaba wamevutiwa na uwepo wa chumba cha mfano cha kuhudumia wagonjwa wanaohitaji uangalizi maalum (ICU) pamoja na mashine maalum ya kupumulia ‘ventilator’.
Mashine hiyo ndiyo ambayo hutumika kusaidia mgonjwa mwenye shida ya upumuaji kuweza kupumua vema baada ya kufanyiwa upasuaji mkubwa ikiwemo upasuaji wa moyo.
Mkazi wa Buguruni, Said Abdallah alisema amefurahi kuona mashine hiyo kwa macho yake, kwani hapo kabla alisikia kwenye vyombo vya habari ikielezwa kwamba ni msaada mkubwa kwa watu wenye shida ya upumuaji.
“Katika kipindi hiki cha Corona, nilisikia wakisema mashine ya ‘ventilator’ inasaidia kuokoa maisha, sasa sikuwa nimewahi kuiona mashine hiyo, ndiyo maana leo unaona nina furaha kubwa, nimeiona hapa kwenye banda la JKCI, SABASABA,” alisema Abdallah.
Kwa upande wake Afisa Uuguzi kutoka JKCI, Mary Haule akizungumza na waandishi wa habari alisema wananchi wengi wamevutiwa na mashine ya ventilator na kuuliza maswali mengi hasa namna gani mashine hiyo inaweza kusaidia kuokoa maisha.
“Sabasaba ya mwaka huu imekuwa ya tofauti katika banda letu tumeweka mfano wa chumba cha ICU, tuna mfano wa binadamu (mdoli) na tumekuja na mashine hii ya ‘ventilator’ tunawaonesha wananchi jinsi tunavyomsaidia mgonjwa aliyetoka katika chumba cha upasuaji na kuwekewa mashine hii kumsaidia kupumua,” alisema Haule.
Aliongeza “Mgonjwa tunayemuhudumia hapa anakuwa bado hajaamka kutoka kwenye dawa ya usingizi, tunamsaidia mpaka hali yake itakapoimarika na kutoka usingizini.
“Hivyo, tunatoa ufahamu kwa wananchi waweze kuelewa kwamba katika Taasisi yetu tuna kitengo cha kusaidia wagonjwa mahututi waliofanyiwa upasuaji na hapa tumekuja tu na baadhi ya mashine kwa ajili ya maonesho, Lakini pale JKCI tunazo zaidi ya mashine 20 za Ventilator, wananchi wamefurahi kuona mfano wa chumba hiki,” alisema Haule
Wakati huo huo Mariam Kaisa ambaye ni Mkazi wa Kiwalani alisema amepata elimu ya kutosha katika banda la JKCI kuhusu lishe na umuhimu wa kufanya mazoezi ili kujikinga dhidi ya magonjwa ya moyo.
“Nimepima afya yangu, nimeambiwa moyo wangu upo vizuri, nimeshauriwa kuzingatia kanuni za afya hasa ulaji unaofaa na mtindo bora wa maisha ili nizidi kulinda afya ya moyo wangu,” alisema Mariam.