Mwenyekiti wa elimu ya Amani Tanzania mkoa wa Kagera Alhajj Maurid Rashid Kambuga akitoa mafunzo ya elimu ya Amani kwa Wananchi,viongozi wa dini,viongozi wa vyama vya siasa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watendaji wengine katika kata ya Rubale.
Wananchi,viongozi wa dini,viongozi wa vyama vya siasa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watendaji wengine katika kata ya Rubale wakiwasikiliza viongozi wa shirika la elimu ya Amani Tanzania waliofika kuwapa elimu ya Amani leo julai 09,2020 katika kijiji cha Rubale.
Wananchi,viongozi wa dini,viongozi wa vyama vya siasa, wenyeviti wa vijiji na vitongoji na watendaji wengine katika kata ya Rubale wakiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa shirika la Amani Tanzania Mkoa Kagera mara baada ya mafunzo.
Picha zote na Allawi Kaboyo.
************************
Na Allawi Kaboyo Bukoba.
Wananchi wa kijiji cha Rubale halmashauri ya wilaya Bukoba Mkoani Kagera wameliomba shirika la Amani Tanzania kuendelea kutoa elimu ya Amani ili kuweza kupunguza vitendo vya uhalifu na uvunjifu wa Amani hasa katika kipindi hiki ambacho nchi inaelekea kwenye uchaguzi mkuu.
Wameyasema hayo katika semina iliyowakutanisha na viongozi wa elimu ya Amani mkoa wa kagera, wenyeviti wa vijiji, wenyeviti wa vitongoji, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na watendaji wengine wa kata ya Rubale leo julai 9,2020 katika kijiji cha Rubale.
Wamesema kuwa jamii imekuwa ikiingia katika mambo yasiyokuwa ya msingi na kupelekea uvunjifu wa mani kwa kutokuwa na elimu juu ya viashiria vinavyosababisha uvunjifu wa Amani na kulishukuru shirika la Amani lililowafikia na kuwapa elimu hiyo huku wakiahidi kuyaishi yote waliyofundishwa na kuwafundisha wengine.
Sheikhe Idd Bashange ni kiongozi wa dini katika kijiji hicho ambapo amesema kuwa ujio wa shirika hilo umewaamsha kiakili na kuwakumbusha wajibu wao kama viongozi wa dini ni nini wanatakiwa kufanya katika kuwahudumia waumini wao hasa katika suala zima la kuhubili Amani.
“Elimu tunayoipata tunatakiwa kuitenga kwa makundi matatu, moja tunatakiwa kumjua mungu, imaani yangu inanituma tukimtambua mungu katika kila kipengele cha maisha yetu Amani itatawala, lakini elimu yapi tunayotakiwa kuwa nayo ni kuwatambua wazazi wawili, tukiwatambua na kuwaheshimu basi Amani itatawala, na elimu ya tatu ni elimu tutakayoipata ikatusaidia namna ya kuishi kwenye jamii yetu inayotuzungaka haya yote tukiyazingatia Amani itashamili kila mahala.” Amesema Sheikhe Bashange.
Mchungaji Devis Kazaula ni mchungaji wa kanisa la P.A.G Rubale amesema kuwa viongozi wa dini wamepata bahati kubwa ya kukutana na shirika la elimu ya Amani hivyo wanawajibika kama viongozi kuifikisha elimu waliyoipata kwa waumini wao ili kuhakikisha kila mtanzania anaishi kwa Amani na kuilinda Amani popote atakapokuwa.
Kazaula ameongeza kuwa viashiria vya uvunjifu wa Amani katika jamii husababishwa ukosefu wa maadili kuanzia kwa wazazi wanaoshindwa kuwa walezi na mifano bora kwa watoto wao na kuwasihi wazazi kutojisahau maana kila kukicha dunia inabadirika hivyo elimu ya Amani ni muhimu kwa wazazi kuanzia ngazi ya familia hadi jamii nzima.
“Vipo vitendo vingi vya uvunjifu wa Amani na vingi husababishwa na kutoweka kwa maadili hasa kwa vijana wetu, niwaombe wazazi shirika hili limekuja kama mkombozi kwetu hasa tunapoelekea katika uchaguzi, tuwasihi vijana wetu wasitumike katika kuvunja Amani mimi ninaamini wote hapa tukijua nini maana ya Amani hata polisi watakuwa hawana kazi za kufanya maa watu wote tutakuwa Raia wema katika nchi yetu.” Amesema Mchungaji Kazaula.
Kwaupande wake mwenyekiti wa shirika la Amani Tanzania Mkoa wa Kagera Alhaji Maurid Rashid Kambuga amewaeleza wananchi pamoja na viongozi hao vitu vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa Amani kuwa ni uwepo wa Rushwa, Ulevi, chuki,Lamri chonganishi, Dhuluma n.k.
Kambuga amesema kuwa elimu ya Amani ni nyenzo kuu muhimu katika kujenga uchumi wan chi yoyote duniani na kuongeza kuwa pindi Amani itakapovunjika basi gharama ya kuirejesha itakuwa kubwa sana na kuwataka wananchi kuilinda na kuwa na wivu wa Amani iliyopo hapa nchini.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha uchaguzi wananchi wanatakiwa kuwa makini Zaidi ili kutokuwa sababu ya uvunjifu wa Amani na kutoa taarifa kwa vyombo husika pale vinapotokea vitendo au viashiria vya uvunjifu wa Amani huku akiwasisitiza kuiogopa na kuipinga rushwa kwa kuwa inauza haki zao na kupelekea uvunjifu wa Amani.
“Tunaingia kwenye kipindi cha uchaguzi watakuja wanansiasa wengi wakiwa na seara zao lakini wapo watakaokuja na pesa zao wakitaka muwachagueni, niwaombe ndugu zangu msiuze haki na utu wenu kwa fedha kidogo ambapo mnakwenda kuyaghalimu maisha yenu yote, Rushwa ni adui namba moja wa haki hivyo niwaombe tusikubali kupokea wala kutoa Rushwa na mtambue pia vitendo vya Rushwa ni viashiria vya uvunjifu wa Amani.” Anesena Alhajj Kambuga.
Ameongeza kuwa viongozi wasiwe sehemu ya uvunjifu wa Amani na badara yake wao wanatakiwa kuwahubiri waumini wao suala zima la Amani pamoja na kuepuka viashiria vya uvunjifu wa Amani nchini.
Akiongea kwaniaba ya mkuu wa kituo cha polisi Rubale PC Ally Mohamed amesema kuwa wamekuwa wakipokea kesi za hovyo kutoka maeneo mbalimbali ambazo nyingi hazina msingi na kulishukuru shirika hilo kwa kutoa elimu ya Amani amabayo amesema kuwa itakuwa chachu kubwa ya mabadiriko katika jamii na kuacha vitendo vya uhalifu.
Ameongeza kuwa “Narishukuru shirika hili kwanza nimefarijika kuwaoneni hapa maana nyinyi ni wadau wakubwa kwetu, hapa kuna vijikesi vya hovyo hadi mtu unajiuliza watu hawa hawana elimu wala ufahamu wa masuala Fulani, mimi nina uhakika kwa elimu mnayoitoa hii jamii itabadirika na kuwa raia wema na sisi tutatoa ushirikiano wa hali ya juu kwenu viongozi ili kuahakikisha elimu hii inawafikia wananchi na mimi kuanzia leo najiunga kuwa mwananchama wa shirika hili.” Amesema Afande Ally.
Ameliomba shirika kuwa elimu hii isiwe ya msimu na badala yake iwe elimu endelevu katika jamii ili kuweza kuleta mwelekeo mzuri katika jamii na kuisaidia serikali kuacha kutumia rasilimali fedha katika kuwatunza na wafungwa na kuendesha mashauri mahakamani.
Baada ya semina hiyo viongozi waliokuwepo katika semina hiyo wameonyeshwa kuwiwa kujiunga na shirika la elimu ya Amani baada ya kuelewa nini maana ya Amani na vitu gani wanatakiwa kuvifanya ili kuilinda, kuihubiri Amani ya Tanzania.