Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akivuta utepe pamoja na Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa ili kuzindua mradi mkubwa wa maji wa Kibamba-Kisarawe katika sherehe zilizofanyika Wilayani Kisarawe Mkoani Pwani leo tarehe 28 Juni 2020.
- Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. John Pombe Magufuli akifungua bomba kwa pamoja na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Maji Profesa Makame Mbarawa, Waziri wa TAMISEMI Selemani Jafo, Naibu Waziri wa Maji Jumaa Aweso, Mtendaji Mkuu wa Dawasa Eng. Cyprian Luhemeja, Mwenyekiti wa Bodi ya Dawasa Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange.
- …………………………………………………………..
Na Erick Msuya MAELEZO DAR ES SALAAM
RAIS Dkt. John Magufuli amezindua mradi mkubwa wa maji wa Kibamba-Kisarawe katika Wilaya ya Kisarawe Mkoani wenye thamani ya Tsh. Bilioni 10.6 ambao umekusudia kuondoa tatizo la ukosefu wa maji lililodumu katika Wilaya hiyo kwa zaidi ya miaka 113 sasa.
Wilaya ya kisarawe sasa inapata maji lita Milioni 6 ukiwa ni mradi wenye dhamani ya bilioni 10.6 fedha za ndani za Dawasco.
Akizungumza katika hafla ya Uzinduzi wa mradi huo unaotekelezwa na Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Jijini Dar es Salaam (DAWASA) leo Jumapili (Juni 28, 2020)kutoka Kibamba hadi Kisarawe, Rais Magufuli alisema kuwepo kwa mradi huo kumekuwa fursa kwa wakazi wa kisarawe kwa kupata ajira pamoja na maji safi.
“Nilipokuwa nazindua mradi wa maji huko mlandizi iliniumiza na kunisikitisha kuona wilaya kongwe kama hii katika Tanzania yenye miaka 113 ikae bila maji, ndo maana nikaamulisha maji lazima yafike kisarawe” alisema Rais Magufuli
Aidha Rais Magufuli alipongeza DAWASA kwa kutanguliza uzalendo wao mbele katika ukusanyaji wa mapato ya bili za maji, na kufikisha huduma bora kwa wateja na kusimamia ipasavyo mradi huo mkubwa wa maji na miradi mingine katika mkoa wa Pwani.
Akifafanua zaidi Rais Magufuli pia aliusifu utendaji kazi wa watumishi wote wa mkoa wa Pwani kwa hatua kubwa inayopiga kimaendeleo kwa kuendelea kusimamia na kuwa wazalendo katika miradi usimamizi wa miradi 45 ya maji iyopo mkoani humo, huku akibainisha zaidi ya Tsh. Bilioni 30.37 zikitolewa mkoani humo kwa ajili ya kugharamia Elimu Bure katika shule za msingi na sekondari.
Kuhusu huduma za afya, Rais Magufuli alisema Serikali imeupatia Mkoa wa Pwani jumla ya magari ya wagonjwa 36 kutoka magari 12 yaliyokuwapo hapo awali, huku jumla ya Tsh. Bilioni 12.8 zikiwa zimetolewa mkoani humo kwa ajili ya kuboresha sekta ya afya na vifaa tiba kwa wananchi.
Akigusia sekta ya Viwanda, Rais Magufuli Mkoa wa Viwanda unaongoza nchini kwa kuwa na idadi kubwa ya viwanda ambapo hadi sasa, una viwanda vikubwa 69, viwanda vya kati 88, viwanda vidogo 216 na viwanda vidogo sana 819 hivyo kuufanya mkoa wa Pwani kuongoza Tanzania kuwa na Viwanda vingi kuliko Mkoa wowote nchini.
“Unapokuwa na viwanda maana yake ushatengeneza ajira, unapokuwa na viwanda hata haya maji ya mradi huu utakaokuwa unatoa maji lita Milioni 6, lakini yanayo hitajika hapa hapa wilayani kisarawe ni lita milioni 1 hivyo viwanda vitasaidia sana hata katika bili ya kulipa maji” alisema rais Magufuli.
Naye Waziri wa Maji, Prof. Makame Mbarawa alisema DAWASA tangu mwezi Juni 2018 ilikuwa inakusanya Bilioni 7.8 kwa mwezi, huku mwezi machi mwaka huu ikikusanya Tsh. Bilioni 12.5 hivyo kuifanya DAWASA kuwa na ongezeko la ukusanyaji bili kufikia asilimia 57.6 ya malengo iliyojiwekea.
Waziri Mbarawa pia alimhakikishia Rais Magufuli kuwa DAWASA itaendelea kukusanya mapato zaidi na katika kipindi cha muda mchache baada ya kukamilika kwa miradi mbalimbali ya maji, DAWASA itakuwa ina uwezo wa kukusanya bilioni 15 kwa mwezi.