*********************
Tarehe 12 Juni ya kila mwaka ni Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ajira kwa Mtoto Duniani – World Day against Child Labour. Siku hii ilianzishwa na Shirika la Kazi Duniani (ILO) mwaka 2002 kwa madhumuni ya kutoa elimu na kufanya uchechemuzi ili kuzuia utumikishwaji kwa watoto.
Shirika la Kazi Duniani kupitia Mkataba wa Kimataifa Na. 138, uliweka umri wa ajira kuwa ni miaka 15 na kuendelea, na Mkataba Na. 182 uliorodhesha ajira zisizokubalika kwa watoto na ambazo zinatakiwa kuzuiwa.
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) inaungana na wadau mbalimbali wa haki za mtoto duniani katika maadhimisho ya siku hii maalum ya kupinga ajira kwa watoto, sambamba na kuelimisha jamii juu ya madhara ya ajira hizo. Kauli mbiu ya maadhimisho haya mwaka huu ni “Gonjwa la COVID-19: Walinde watoto dhidi ya ajira kwa watoto, sasa kuliko wakati mwingine wowote – COVID-19: Protect children from child labour, now more than ever.”
Tunapoadhimisha siku hii, THBUB inaendelea kuihamasisha jamii kuheshimu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya Mwaka 1977, Sheria, Sera, Mipango na melekezo mbalimbali yanayolinda haki za mtoto nchini.
Sheria ya Mtoto Sura ya 13 inamtambua mtoto kuwa ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18. Kifungu cha 12 cha Sheria hii kinaelekeza kuwa, mtoto hatahusishwa katika kazi yoyote ambayo inaweza kumsababishia madhara kiafya, kielimu, kiakili, kimwili na katika ukuaji wake. Aidha, Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura ya 366 inaelekeza wazi kuwa mtoto ataajiriwa katika kazi zinazofaa ambazo siyo ngumu na zisizoathiri mahudhurio yake shuleni na haki zake nyingine.
Pamoja na uwepo wa sheria, kanuni, mifumo na miongozo inayowalinda watoto, bado zipo changamoto kadhaa,zikiwemo watoto kufanyishwa kazi ngumu na zisizofaa, tena katika umri ambao hauruhusiwi kisheria, na mara nyingine zaidi ya muda uliowekwa kisheria.
Tafiti zinaonesha kuwa hapa nchini, ajira za watoto ziko katika maeneo ya kazi za ndani, mashambani, mitaani, na migodini. Ajira hizi zimekuwa kichocheo cha ukatili dhidi ya watoto. Kutokana na tafiti hizo, sababu kubwa ya ajira kwa watoto ni umasikini na kukosa uelewa juu ya madhara ya ajira hizo. Hali hii inawaathiri zaidi watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani; kwani wanahitaji kufanya kazi ili kujikimu. Aidha, watoto wanaofanyishwa kazi wanapitia changamoto nyingi, zikiwemo kukosa masomo, ukatili wa kingono na kimwili, kunyonywa kiuchumi, matatizo ya kiafya na changamoto nyinginezo zinazoathiri ukuaji wao.
Kufuatia kuibuka kwa janga la kidunia la ugonjwa wa COVID-19 unaosababishwa na virusi vya corona, watoto walioko katika ajira hizi wamo hatarini zaidi ya kupata maambukizi. Hivyo, jumuiya ya kimataifa imelipa kipaumbele suala la ulinzi kwa watoto dhidi ya ajira hatarishi.
Ni kwa muktadha huo, THBUB ikishirikiana na wadau mbalimbali inaendelea kuihamasisha jamii kuwalinda zaidi watoto dhidi ya ajira hatarishi sasa kuliko wakati mwingine wowote. Hii ni kwa sababu watoto ndio waathirika wakubwa kunapozuka majanga mbalimbali, ikiwemo gonjwa la COVID-19.
Kwa namna ya kipekee, THBUB inatambua na kuzipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa jitihada mbali mbali wanazochukuwa katika kukabiliana na ugonjwa huu na hivyo kupunguza athari kubwa kwa watoto nchini.
Hivyo, tunapoadhimisha Siku ya kupinga ajira kwa watoto, na kwa kutambua madhara ya janga la COVID-19, THBUB inatoa wito kwa umma, Serikali na wadau wa haki za watoto kuunganisha nguvu kupinga ajira kwa watoto mahali popote nchini. Aidha, Tume inapendekeza yafuatayo:
- Taasisi zinazohusika na usimamizi na utekelezaji wa sheria za kazi zisimamie ipasavyo sheria za kazi ili kuzuia utumikishwaji kwa watoto katika ajira zisizo halali ikiwa ni pamoja na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara katika maeneo ya kazi;
- Serikali zote mbili kwa kushirikiana na wadau ziendelee na jitihada za kutoa elimu ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona;
- Serikali kwa kushirikiana na wadau wa elimu ziendelee kuwasaidia watoto wanaoishi na kufanya kazi mitaani kurejea shule kwa kujenga mifumo bora itakayowawezesha kupata mahitaji yao ya kila siku.
- Serikali iendeleze na kuboresha jitihada mbalimbali zinazochukuliwa kuwabainisha wanaowaajiri watoto na kuwawajibisha kisheria. Pia jamii iendelee kutoa ushirikiano kwa kuwafichua watu wote wanaowaajiri watoto.
- Wazazi wahakikishe wanawatunza, kuwalinda na kuwapatia watoto mahitaji yao ya msingi. Aidha, wahakikishe watoto wote wanahudhuria shule na hawawatumii kama vitega uchumi vya familia kwa kuwafanyisha kazi ngumu, zisizofaa na zinazowaathiri.
- Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali iendelee kutoa elimu ya haki za mtoto na madhara ya ajira mbaya kwa watoto.
“Walinde watoto dhidi ya ajira mbaya sasa!”