Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Bw.Gerald Kusaya (aliyevaa t-shirt mistari nya blu) akikagua eneo la ujenzi wa vihenge vya kisasa eneo Ibadakuli Shinyanga.Katibu Mkuu huyo ameeleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi na kutaka mkandarasi aongeze spidi.
…………………………………………………………………………….
Katibu Mkuu Wizara ya Kilimo Gerald Kusaya leo amefanya ziara ya kushtukiza kwenye eneo la ujenzi wa vihenge vya kisasa (silos) mjini Shinyanga na kuelezea kutoridhishwa na kasi ya ujenzi huo .
” Mkandarasi sijaridhishwa na kazi yako kuwa na kasi ndogo wakati serikali inahitaji mradi huu wa maghala ukamilike kwa wakati.Nataka uongeze idadi ya vibarua na mafundi ili spidi ya kazi iongezeke ” alisema Kusaya
Katibu Mkuu huyo ameelekeza mkandarasi kuwa ataendelea kutembelea ujenzi wa vihenge hivyo mara kwa mara bila taarifa kukagua kwani Wizara inataka kuona vihenge na maghala hayo yanakamilika kwa wakati kwa ajili ya kuhifadhi mazao ya chakula kwa matumizi ya Taifa.
Kusaya alibainisha kuwa serikali inatekeleza mradi huo mkubwa wa shilingi Bilioni 15.24 wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi kwa kujenga vihenge (silos) sita zenye uwezo wa kuhifadhi tani 20,000 na ghala moja kubwa lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka katika eneo la Ibadakuli mkoani Shinyanga.
Katibu Mkuu Kusaya alikuwa njiani kutoka Mwanza kuelekea Dodoma aliposimama mkoani Shinyanga kukagua mradi huo wa ujenzi wa vihenge .