Muonekano wa Daraja la Kalamba liliopo Mkoa wa Dodoma, katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa likiwa limekarabatiwa upya baada ya kuharibiwa na mvua, daraja hilo ni kiunganishi ya kata ya Kidulo na Kata ya Kalamba.
Ujenzi wa Kalavati Mstatili (Box culvert), katika barabara ya Bashay- Endaguday- Hydom (inayoelekea Yaedachin wanapopatikana Wahadzabe), ukiwa unaendelea baada ya mawasiliano kukatika kutokana na mvua.
……………………………………………………………………………………………………..
Na.Mwandishi wetu – TARURA
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA), umeendelea kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimballi yaliyoathiriwa na mvua nchini na kusababisha adha kwa watumiaji wa barabara hizo pamoja na madaraja.
Kwa Mikoa ya Dodoma na Manyara, tayari mawasiliano yanaendelea kurejeshwa kwa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu, Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mji na Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa.
Meneja wa Wakala Wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Babati Mhandisi Said Mikongomi ameeleza kuwa tayari wamerejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali na sasa wananchi wanaendelea na shughuli zao za kiuchumi.
‘‘Tumeanza kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali ili wananchi waweze kupita na kuendelea na shughuli zao za kiuchumi, maeneo yaliyorekebishwa ni Pamoja na Daraja la Masware ambalo tayari linapitika na Daraja hili pia linapitisha malighafi zinazoenda katika kiwanda cha sukari cha Babati’’.
Naye, Bw. Domini Mao ambaye ni mkazi wa mtaa wa Matufa amesema kuwa wananchi walipata shida sana kuvuka daraja la Masware baada ya ukuta wa daraja hilo kuanguka lakini kwa sasa tayari ukuta huo umerejeshwa na hivyo wanapita vizuri na kazi zinaendelea kufanyika kwa urahisi.
“Tunawashukuru sana TARURA kurejesha mawasiliano katika daraja hili kwani hili ni daraja la muhimu kwetu kwani tunapitisha mazao lakini pia malighafi zinazopelekwa katika kiwanda cha sukari cha Babati’’.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu mawasiliano pia yamerejeshwa na wananchi wanapita kwa urahisi, akizungumza katika mahojiano maalum, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Hudson Kamoga ameeleza kuwa maeneo yaliyoharibiwa na mvua tayari yanapitika.
Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa kazi zinazofanywa na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA zimeleta mageuzi makubwa kwa wananchi kwani wataalamu wa TARURA wanafika mapema sana pale changamoto inapotokea na wananchi wanaona moja kwa moja jinsi serikali inavyo wahudumia.
‘‘Nichukue fursa hii kumpongeza Rais wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Serikali kwa ujumla kwa kuanzisha TARURA, hivi saa wataalamu hawa wa TARURA wapo karibu sana na wananchi na wanachukua hatua mapema kurejesha mawasiliano pale inapotokea changamoto hasa kwa kipindi hiki ambacho mvua zimekuwa kubwa sana’’.
Meneja wa Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbulu Mhandisi Nuru Hondo ameeleza kuwa katika Halmashauri hiyo, kazi zinaendelea kufanyika ili kurejesha mawasiliano na tayari maeneo mengi yaliyoharibiwa na mvua yanapitika.
Katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa mkoani Dodoma, mawasiliano pia yamerejeshwa ambapo daraja la Kalamba tayari limefanyiwa matengenezo na wananchi wanavuka bila shida.
Akizungumza katika mahojiano malum, Meneja wa TARURA katika Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa Mhandisi Goodluck Mbanga ameeleza kuwa mvua zilizonyesha zilikata mawasiliano katika Daraja la Kalamba lakini hadi sasa tayari matengenezo yamefanyika na wananchi wanasafiri bila shida huku akifafanua kuwa matengenezo makubwa yataendelea kufanyika kwa mwaka wa fedha ujao.
Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini TARURA unaendelea kurejesha mawasiliano katika maeneo mbalimbali nchini baada ya mvua kunyesha kwa muda mrefu na kusababisha baadhi ya maeneo kutopitika.