Home Mchanganyiko VYAMA VYA USHIRIKA VYA SHAURIWA KUTUNZA AKIBA ILI KUWEZA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO...

VYAMA VYA USHIRIKA VYA SHAURIWA KUTUNZA AKIBA ILI KUWEZA KUTATUA CHANGAMOTO ZAO KIMAISHA

0
Wakulima wa Vyama vya Ushirika nchini wamepewa wito wa kuboresha maisha yao kwa
kuweka akiba baada ya msimu wa mavuno ya mazao yao ili akiba hizo ziwasaidie hususan wanapopata changamoto mbalimbali za kimaisha.
Wito
huo umetolewa na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume
ya Maendeleo ya Ushirika (TCDC) Dkt. Benson Ndiege wakati alipotembelea
Chama cha Ushirika wa Wakulima wadogo wadogo wa Kilimo cha umwagiliaji
Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA LTD) kwenye ziara ya Kikazi, Mkoani Morogoro
hivi karibuni.

Mrajis amesema kuwa wanachama wa Ushirika
wanaweza kutumia fursa ya kuwa pamoja katika Chama kwa kuimarisha
Ushirika wao kwa kujiwekea utaratibu maalum wa kutunza akiba
zinazotokana na mauzo ya mazao pale wanapovuna. Alibainisha kuwa
utaratibu huo utakaposimamiwa vizuri kwa taratibu za kiushirika unaweza
kuongeza fursa nyingine ya kuwa na Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo
(SACCOS) inayotokana na wanachama wa UWAWAKUDA.

“Kila mkulima
anapovuna anaweza kujiwekea Akiba katika Mfuko wao ambao utatumiwa na
Wanaushirika kwa mahitaji yao mbalimbali pamoja na dharura
zinapojitokeza kwa mwanachama,” alisema Mrajis

Aidha, Akielezea
Chama hicho Mwenyekiti wa UWAWAKUDA Bw. Thomas Kalema alisema kuwa Chama
hicho cha Ushirika chenye jumla ya Eka 5,000 za umwagiliaji
kilianzishwa rasmi tarehe 24 Julai 2006 kina Jumla ya Wanachama 935
ambao kati ya hao 552 ni wanaume, 376 ni wanawake pamoja taasisi za
kidini 7. Alibainisha kuwa Mradi huo umekuwa ukipata ufadhili kutoka
Serikalini pamoja na wadau wengine wa maendeleo kwa lengo la kuwakomboa
wananchi kiuchumi.

Makamu Mwenyekiti wa Chama hicho Bertha
Chilosa alipata fursa ya kueleza kuwa kabla ya kuanzishwa kwa Ushirika
miaka ya 2004 kurudi nyuma, hali ya maisha ya wakazi wa Dakawa ilikuwa
duni sana ukilinanisha na baada ya Ushirika kuanzishwa. Alibainisha
baadhi ya manufaa yaliyopatikana na mradi huo ni pamoja na Wanachama
wengi kuweza kujenga nyumba bora za kisasa, fursa za mikopo kwenye
taasisi za kifedha, huduma kwa jamii, upatikanaji wa ajira akitoa mfano
kuwa zaidi ya vibarua 5,000 kutoka Dakawa na maeneo jirani katika
kipindi cha msimu wa kilimo. Aliongeza kuwa vijana wengi kupitia shamba
la UWAWAKUDA wamefungua biashara mbalimbali zinazowasaidia kuhudumia
familia na kuchangia pato la Taifa.
Mrajis wa Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege (wa pili kulia) akipata
maelezo ya Shamba la Skimu ya Umwagiliaji ya Chama cha Ushirika cha
Wakulima Wadogo wadogo wa Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA) kutoka kwa
Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Thomas Kalema, hivi karibuni alipokuwa
kwenye ziara ya kikazi Mkoani Morogoro.
 Makamu
Mwenyekiti wa Chama cha Ushirika (UWAWAKUDA) Bertha Chilosa akitoa
maelezo kuhusu Mradi wa Shamba la mpunga la Chama hicho kwa Mrajis wa
Vyama vya Ushirika Dkt. Benson Ndiege, katikati ni Mwenyekiti wa Chama
Bw. Thomas Kalema akifuatiwa na Afisa Ushirika Dawson Kikalugaa, Mkoani
Morogoro .

 Muonekano wa Shamba la Skimu ya Umwagiliaji ya Chama cha Ushirika cha Wakulima Wadogo wadogo wa Mpunga Dakawa (UWAWAKUDA) .


 Magunia ya Mpunga yakiwa katika hatua za maandalizi kutoka Shamba la Mpunga la UWAWAKUDA
 Mrajis
Dkt. Benson Ndiege akioneshwa mitambo ya Pampu za maji za mradi wa
Skimu ya Umwagiliaji wa UWAWAKUDA, Dakawa Mkoani Morogoro