Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akipiga makofi baada ya kuzindua Kituo cha Afya Sunya, kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akizindua Kituo cha Afya Sunya, kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akiongea na watumishi Kituo cha Afya Sunya, wakati wa uzinduzi wa kituo hicho kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akikagua vifaa vya vilivyopo katika Kituo cha Afya Sunya, kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Mhe.Selemani Jafo akizungumza na uongozi wa Halmashauri ya wilaya Kiteto leo katika ukaguzi wa jengo la utawala la halmashauri hiyo.
……………………………………………………………………
Na. Majid Abdulkarim , Kiteto
WAZIRI wa Nchi,Ofisi ya Rais,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI), Selemani Jafo amewataka wataalam wa afya kujipanga vema katika kutoa huduma nzuri kwa wananchi ili kutimiza adhima ya Mhe.Rais ya kuwatumikia watanzania.
Kauli hiyo ameitoa leo wakati wa uzinduzi wa kituo cha afya cha Sunya kilichopo wilayani Kiteto Mkoani Manyara.
Aidha Mhe. Jafo amewataka wananchi kuhakikisha wanalinda miundombinu ya kituo hicho ili dhamira ya serikali ya kusogeza huduma za afya karibu na wananchi iweze kutimizwa .
Katika uzinduzi huo Mhe.Jafo amesema kituo hicho ndani ya wilaya hiyo kitakuwa msaada mkubwa sana kwa wananchi wa hapo na kitakuwa kimetatua changamoto nyingi ikiwemo kukosekana kwa kituo cha afya katika kata ya Sunya hali iliyowalazimu wakazi hao kusafiri umbali mrefu.
“ukosefu wa kituo cha afya katika kata hii kulilazimu wananchi kwenda wilayani Kilindi mkoani Tanga au kusafiri kilomita 125 kufuata huduma katika hospitali ya wilaya,”ameleza Mhe. Jafo.
Akizungumza Mhe.Jafo amesema kuwa kituo hicho ni miongoni mwa vituo vilivyopewa kiasi cha shilingi milioni 400 na ujenzi umekamilika kwa kiwango alichoridhika nacho.
“Niwaombe wananchi mshirikiane katika kutunza miundombinu ya kituo hiki,sitarajii nikija hapa nikute mmeharibu koki hapana,kila mtu awe mlinzi wa mwenzake ili kituo hiki kiwe na manufaa kwa sisi na vizazi vyetu vijavyo,”ametoa wito Mhe. Jafo.
Katika hatua nyingine pia Mhe. Jafo amekagua ujenzi wa jengo la halmashauri na kumtaka mkandarasi wa Pacha Construction LTD kukamilisha ujenzi kwa wakati uliyopangwa.
“Mkurugenzi ninachosisitiza hapa kazi ikamilike kwa wakati na niwaambie hili jengo likikamilika litakuwa ni miongoni mwa halmashauri zenye ofisi nzuri nchini,lakini wakati mwingine jitahidi gharama ziwe ndogo tofauti na hizi za sasa hivi,”ameelekeza Mhe. Jafo.
Naye Mkuu wa wilaya hiyo Mhe.Tumaini Magese ameiomba serikali kuwaongezea vituo vya afya viwili ili kurahisisha upatikanaji wa huduma za afya kutokana na ukubwa wa wilaya hiyo.
Mhe. Magesa amebainisha changamoto iliyopo kwa sasa katika kituo hicho kuwa ni ukosefu wa umeme na hivyo kulazimika kutumia jenereta.
“Wilaya hii ni kubwa ina tarafa saba na imetawanyika sana,niiombe serikali itakapopatikana fursa basi tupate vituo vingine viwili ili visaidie wananchi wetu,suala la umeme bado ni changamoto,waziri wa nishati alikuja ameridhia kuleta umeme hivyo tunasubiria,”ameeleza Mhe. Magese
Akitoa taarifa ya ujenzi huo Mkurugenzi wa halmashauri ya Kiteto Tamimu Kambona amesema kuwa ujenzi huo ulianza januari 2018 na umekamilika mwaka 2019 kwa gharama ya zaidi ya shilingi milioni 510 na wananchi elfu 38,273 wanatarajiwa kupata huduma katika kituo hicho.
Kambona amesema kuwa fedha zilizotumika ni shilingi milioni 483.4 na kiasi cha milioni 35 ni bakaa ambazo zitatumika kwa ajili ya kujenga duka la dawa.
“Uwepo wa kituo hiki utasaidia kuondoa adha ya kutembea umbali mrefu waliyokuwa wanapata wananchi pindi walipotaka huduma za afya lakini pia kutapunguza vifo vya mama wajawazito na watoto,”ameeleza Kambona
Awali akizungumza katika uzinduzi huo mbunge wa Kiteto Emmanuel Papian kwa niaba ya wananchi ameishukuru serikali kwa kukamilisha kituo hicho na kumuomba waziri afikishe salamu zao kwa Rais Dkt John Magufuli.