Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali imeendelea kuiweka sekta ya elimu miongoni mwa vipaumbele vyake vya maendeleo, ikitambua kuwa uwekezaji katika elimu ni msingi wa kuimarisha uwezo wa wananchi, kuongeza ushindani wa uchumi na kujenga mustakabali bora wa taifa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 25 Novemba 2026, katika Mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (Zanzibar University), Tunguu. Amesema dhamira hiyo inaendana na utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ya mwaka 2025–2030 inayosisitiza ujenzi wa uchumi imara, jumuishi na wenye ushindani unaotegemea maarifa, ujuzi, sayansi, teknolojia na ubunifu.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeendelea kuwekeza katika kuboresha miundombinu ya elimu kuanzia ngazi ya maandalizi hadi elimu ya juu, ikiwemo ujenzi na ukarabati wa madarasa, maabara, maktaba na miundombinu mingine ya kufundishia na kujifunzia. Hatua hiyo inalenga kupanua fursa za elimu na kuongeza idadi ya wanafunzi wanaopata sifa za kuendelea na elimu ya juu.
Ameeleza kuwa ongezeko la fursa hizo linaongeza wajibu kwa vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kujiandaa kukidhi mahitaji yanayoongezeka, sambamba na kuhakikisha viwango vya ubora wa elimu vinadumishwa na kuimarishwa.
Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali pia inaendelea kuongeza fedha kwa ajili ya mikopo ya elimu ya juu na kutoa ufadhili kwa wanafunzi wenye ufaulu wa juu, ili kupunguza changamoto za kifedha zinazoweza kuwazuia vijana wenye sifa kuendelea na masomo.
Ameeleza kuwa kuanzia mwaka wa fedha ujao, Serikali itaanza kutoa ufadhili kwa wanafunzi wote watakaopata Daraja la Kwanza kwa pointi 3 hadi 5 katika mitihani ya Kidato cha Sita, hatua itakayopanua zaidi fursa za elimu ya juu kwa vijana.
Katika hatua nyingine, Rais Dkt. Mwinyi amevitaka vyuo vikuu kuimarisha tafiti, ubunifu na uvumbuzi badala ya kujikita katika ufundishaji na utoaji wa vyeti vya kitaaluma pekee.
Amesema tafiti zinapaswa kuelekezwa katika maeneo muhimu ya maendeleo ya taifa, yakiwemo Uchumi wa Buluu, kilimo, afya, mabadiliko ya tabianchi, nishati mbadala, sayansi na teknolojia, ili kuzalisha maarifa na suluhisho zitakazosaidia kukabiliana na changamoto za jamii.
Pia ametoa wito kwa Chuo Kikuu cha Zanzibar na taasisi nyingine za elimu ya juu kuwekeza katika wahadhiri wenye sifa stahiki, miundombinu ya kisasa ya kufundishia na kujifunzia, maabara, maktaba pamoja na mifumo madhubuti ya uthibiti wa ubora wa elimu.
Akizungumzia utekelezaji wa Dira ya Maendeleo ya Zanzibar ya mwaka 2050, Rais Dkt. Mwinyi amesema taifa linahitaji rasilimali watu wenye maarifa, ujuzi, maadili na uwezo wa kutumia teknolojia katika uzalishaji na ubunifu ili kufikia malengo ya maendeleo yaliyowekwa.
Amesema vyuo vikuu vina wajibu wa kuandaa programu za masomo zinazoendana na vipaumbele vya maendeleo ya taifa na mahitaji ya soko la ajira, pamoja na kuimarisha ushirikiano na waajiri ili kuwawezesha wahitimu kupata maarifa ya kitaaluma na ujuzi wa vitendo unaohitajika katika maeneo ya kazi.
Akitoa nasaha kwa wahitimu, Rais Dkt. Mwinyi amewataka kuzingatia uadilifu, weledi, nidhamu, uwajibikaji na kuheshimu utawala wa sheria wanapoingia katika sekta ya umma na binafsi. Amesisitiza kuwa vyeti vya kitaaluma si dhamana ya moja kwa moja ya kupata ajira, bali ni msingi wa kujenga taaluma na kuchangia maendeleo ya jamii.
Kwa wahitimu kutoka nje ya Tanzania, Rais Dkt. Mwinyi amewataka kuwa mabalozi wazuri wa Zanzibar katika mataifa yao kwa kuwahamasisha wengine kuja Zanzibar kwa ajili ya masomo, uwekezaji, biashara na utalii.
Naye Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohammed Mussa, amesema vyuo vikuu Zanzibar vina nafasi muhimu katika utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya taifa kwa kuzalisha wataalamu wenye maarifa na ujuzi unaohitajika katika sekta mbalimbali.
Mhe. Leila amesema ni jambo la kufurahisha kushuhudia wataalamu wakihitimu katika ngazi mbalimbali, zikiwemo Astashahada, Stashahada, Shahada ya Kwanza, Stashahada ya Uzamili na Shahada ya Uzamili.
Katika Mahafali ya 24 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar, jumla ya wahitimu 1,303 kutoka nchi mbalimbali zikiwemo Tanzania, Malawi, Rwanda, Yemen, Zimbabwe na Nigeria wametunukiwa vyeti katika ngazi tofauti za taaluma baada ya kukamilisha programu mbalimbali za masomo.

