Aelekeza miradi ya maji iliyokwama ianze kutekelezwa

………….

WAZIRI MKUU Dkt. Mwigulu Nchemba ametoa siku 30 kwa mkandarasi wa barabara ya Ifakara–Mbingu yenye urefu wa kilometa 62.5 ahakikishe anaanza kazi za ujenzi baada ya Serikali kumlipa fedha za awali za utekelezaji wa mradi huo.

Waziri Mkuu ametoa agizo hilo leo (Jumatano, Novemba 25, 2026) wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Shule ya Msingi Lukolongo, Kata ya Mchombe, Halmashauri ya Wilaya ya Mlimba, mkoani Morogoro.

Amesema hataki kuona mkandarasi akitembelea eneo la mradi bila kufanya kazi, bali wananchi wanapaswa kushuhudia mitambo ikiendelea na ujenzi ifikapo Desemba 25, 2026.

“Ndani ya siku 30 nataka mkandarasi awe anafanya kazi. Siyo kuzungukia saiti. Nataka watu waione kazi. Sasa hivi hakuna kisingizio. TANROADS wanapokea fedha kila mwezi na mkandarasi keshapewa pesa,” amesema.

Dkt. Mwigulu amesema atafuatilia utekelezaji wa agizo hilo na kuitaka Wizara ya Ujenzi impatie taarifa pamoja na picha zinazoonesha mitambo ikiendelea na kazi ifikapo Desemba 25, mwaka huu.

“Tarehe 25 ni sikukuu ya Krismasi lakini nataka nipate taarifa na pia nitumiwe picha nikiona mitambo ikiwa inafanya kazi ya ujenzi wa barabara hiyo. Pesa imeshapatikana, tunataka kazi ifanyike. Wana-Kilombero na wana-Mlimba wanataka barabara,” amesema.

Amesema Serikali inatambua umuhimu wa barabara hiyo katika shughuli za uzalishaji na usafirishaji wa mazao, akisisitiza kuwa kuchelewa kwa utekelezaji wake hakumaanishi kuwa eneo hilo limesahaulika.

“Barabara yenu ni barabara ya kiuchumi. Hii ni barabara ya uzalishaji mali. Hii si barabara ya matembezi. Ni barabara inayotoka kwenye eneo linalochangia chakula, siyo tu kwa wana-Mlimba bali kwa nchi nzima,” amesema.

Mapema, akitoa ufafanuzi kuhusu mradi huo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema mkataba wa ujenzi wa barabara ya Ifakara–Mbingu ulisainiwa mwaka 2023 na mkandarasi ameshalipwa fedha za awali ili kuanza utekelezaji.

Amesema kipande kingine cha barabara hiyo, kutoka Mbingu hadi Chita JKT, chenye urefu wa kilometa 37.5, tayari kina mkandarasi lakini malipo ya awali bado hayajatolewa.

Mhandisi Kasekenya amesema Serikali imepanga kujenga jumla ya kilometa 100 kwa kuanzia upande wa Ifakara kuelekea Mlimba, huku utekelezaji wa kipande kinachounganisha eneo hilo na Mkoa wa Njombe ukisubiri malipo ya awali kwa mkandarasi.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameiagiza Wizara ya Maji ihakikishe fedha zinazotolewa kupitia Mfuko wa Maji zinatumika kuendeleza miradi iliyokwama ili wananchi wapate huduma hiyo.

Amesema anahitaji taarifa ya miradi iliyofufuliwa tangu kuanza kwa mwaka wa fedha 2026/2027 na hatua zinazochukuliwa kuhakikisha fedha zilizotengwa zinatumika kutatua changamoto za upatikanaji wa maji.

“Nataka kuona fedha hizo zikitekeleza miradi hiyo ya maji. Nitahitaji taarifa nione tangu tuanze kupokea ni miradi mingapi tumeshaiamsha ili wananchi hawa wasipate shida ya maji,” amesema.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Maji, Mhandisi Kundo Andrea Mathew, alisema vijiji 46 kati ya 62 vya Mlimba vinapata huduma ya maji safi na salama, huku Serikali ikiendelea na utekelezaji wa miradi ya maji ili kuongeza upatikanaji wa huduma hiyo kutoka asilimia 78 hadi asilimia 85.