Meneja Mwandamizi wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, akizungumza na washiriki wa programu ya Women Empowerment Programme (WEP), wakati wa ufunguzi wa awamu mpya ya mafunzo ya wiki sita yanayoendeshwa na Benki ya Exim Tanzania. Katika awamu hii, wanawake 50 wanaomiliki na kusimamia biashara ndogo na za kati wanapatiwa mafunzo ya usimamizi wa biashara na fedha, upangaji wa bajeti na kukuza masoko, pamoja na ushauri elekezi na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara. Kupitia programu hii iliyo chini ya mpango wa Exim Cares, Benki inalenga kuwawezesha wanawake kuimarisha biashara zao, kuongeza ushindani na kutumia fursa mpya za ukuaji.

……………. 

Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam

BENKI ya Exim Tanzania imezindua awamu nyingine ya mafunzo kupitia programu yake ya Women Empowerment Programme (WEP), itakayowanufaisha wanawake wajasiriamali wengine 50 kwa kuwajengea uwezo wa kusimamia biashara, kuimarisha mifumo ya fedha na kutumia fursa za masoko kwa ajili ya kukuza biashara zao.

Mafunzo hayo yanalenga kuwapatia wanawake wanaomiliki au kusimamia biashara ndogo na za kati maarifa na ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kukabiliana na changamoto za uendeshaji wa biashara na kujenga shughuli za kiuchumi zenye ushindani na endelevu.

Tangu kuanzishwa kwake, programu ya WEP imeendelea kupanua wigo wa kuwafikia wanawake wajasiriamali. Mwaka 2024, programu hiyo ilipanuliwa hadi mkoani Arusha, huku mwaka 2025 maudhui ya mafunzo yakiboreshwa kwa kujumuisha masuala ya uongozi, uimara wa kihisia na ujenzi wa mitandao ya kimkakati ya kibiashara. Kufikia mwaka huo, zaidi ya wanawake wajasiriamali 300 walikuwa wamenufaika na programu hiyo.

Mwaka 2026, Benki ya Exim Tanzania iliimarisha zaidi programu hiyo kupitia ushirikiano na Chemba ya Wanawake Wafanyabiashara Tanzania (TWCC), kwa lengo la kuboresha utekelezaji wake na kuwapa washiriki fursa pana zaidi za kujenga mitandao ya biashara na kukuza shughuli zao. Hatua hiyo imekuja baada ya kundi la kwanza la wanawake 50 kuhitimu mafunzo hayo Septemba mwaka huu.

Mafunzo hayo ya wiki sita yanajikita katika maeneo mbalimbali ya uendeshaji wa biashara, yakiwemo usimamizi wa mapato na matumizi, utunzaji wa kumbukumbu za fedha, uandaaji wa bajeti, udhibiti wa gharama za uendeshaji na upangaji wa bei za bidhaa na hudum

Aidha, washiriki wanapatiwa maarifa ya kutambua fursa za masoko na kuweka mikakati ya kuwafikia wateja wengi zaidi, hatua inayotarajiwa kuwasaidia kuongeza mapato, kusimamia rasilimali zao kwa ufanisi na kufanya maamuzi sahihi ya kibiashara.

Mbali na mafunzo ya darasani, washiriki watanufaika na ushauri elekezi na fursa za kujenga mitandao ya kibiashara zitakazowawezesha kubadilishana uzoefu, kupata mitazamo mipya na kujifunza mbinu za kukabiliana na changamoto zinazokabili biashara zao.

Akizungumza wakati wa ufunguzi rasmi wa mafunzo hayo, Meneja Mkuu wa Masoko na Mawasiliano wa Benki ya Exim Tanzania, Kauthar D’souza, alisema kuwa kuwawezesha wanawake wajasiriamali kunahitaji kuwapatia maarifa na ujuzi wa vitendo utakaowawezesha kusimamia biashara zao kwa ufanisi na kutumia fursa zilizopo kukuza shughuli zao.

Alisema kupitia programu ya WEP, benki inalenga kuimarisha uwezo wa wanawake katika ujasiriamali kwa kuwapatia nyenzo na msaada unaohitajika ili kukabiliana na changamoto za usimamizi wa biashara na kujenga biashara zenye ushindani na zinazoweza kudumu.

Kwa upande wake, Julieth Micky Msofe, mmiliki wa Dream Designs, inayojihusisha na ubunifu na utengenezaji wa mavazi ya wanawake, alisema mafunzo hayo yatampa maarifa zaidi ya kuendesha biashara yake kwa ufanisi, kuboresha mipango ya biashara na kutambua fursa mpya za ukuaji.

Alisema ujuzi wa kusimamia fedha, kudhibiti gharama za uendeshaji na kutafuta masoko ni muhimu katika kuongeza ushindani wa biashara na kuhakikisha inakua na kudumu.

Naye Irene Modesta Kambewe, mmiliki wa MIMII Quality Products, alisema mafunzo hayo yatamsaidia kuongeza uelewa kuhusu usimamizi wa fedha, utunzaji wa kumbukumbu na uandaaji wa mikakati ya kukuza biashara.

Aliongeza kuwa maarifa atakayoyapata yatakuwa muhimu katika kuimarisha shughuli zake za kibiashara na kumwezesha kutumia fursa mpya zitakazojitokeza.

Kupitia programu hiyo, Benki ya Exim Tanzania inaendelea kuwekeza katika maarifa na uwezo wa wanawake wajasiriamali, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuwawezesha kujenga biashara imara zinazoweza kuhimili changamoto, kuzalisha ajira na kuchangia maendeleo ya uchumi wa Tanzania.