Wajumbe wa Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi hiyo Mhandisi Richard Mbilinyi (kushoto), wakipata maelezo kuhusu utekelezaji wa miradi 12 inayotekelezwa katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini kutoka kwa Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja (kulia), wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya miradi hiyo mkoani Mbeya.

……….
Bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme (ETDCO), ikiongozwa na Mwenyekiti wake, Mhandisi Richard Mbilinyi, imeanza ziara ya kukagua maendeleo ya utekelezaji wa miradi ya miundombinu ya umeme katika Kanda ya Nyanda za Juu Kusini yenye thamani ya shilingi bilioni 53.
Akizungumza Novemba 21, 2026, mkoani Mbeya, Mhandisi Mbilinyi amesema ziara hiyo inalenga kutathmini utekelezaji wa miradi 12 inayotekelezwa katika mikoa ya Mbeya, Songwe, Iringa na Njombe.
Mhandisi Mbilinyi amesema Bodi imeridhishwa na hatua iliyofikiwa katika utekelezaji wa miradi hiyo, huku baadhi ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilika.
“Kukamilika kwa miradi hii kutaimarisha upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika kwa wananchi na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika mikoa husika” amesema Mhandisi Mbilinyi.
Aidha, utekelezaji wa miradi hiyo umewezesha wananchi 450 kupata ajira katika maeneo mbalimbali, hatua inayochangia kuongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Mhandisi Richard Mwanja, amesema kampuni hiyo inatekeleza miradi kwa mikataba na Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) na Wakala wa Nishati Vijijini (REA), ikiwa ni juhudi za Serikali za kuboresha miundombinu ya umeme na kuongeza uhakika wa upatikanaji wa nishati nchini.
Meneja wa Miradi wa ETDCO Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Mhandisi Ajuaye Jeggo, amesema miradi hiyo imefikia kuanzia asilimia 50 hadi 98 katika utekelezaji wake.
Kwa upande wao, wafanyakazi wanaoshiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo wameishukuru Serikali kupitia ETDCO kwa kuwapatia fursa za ajira, wakisema zimewasaidia kupata kipato na kukidhi mahitaji yao ya kila siku