DODOMA, Novemba 24, 2026 

Tume ya Madini imewahimiza wananchi na wawekezaji wanaokusudia kuwekeza katika sekta ya madini kufuata taratibu zilizowekwa za upatikanaji wa leseni na kutekeleza masharti yake ili kunufaika na fursa mbalimbali za uwekezaji zilizopo nchini.

Wito huo umetolewa leo na Mkurugenzi wa Leseni wa Tume ya Madini, Eng. Aziza Swedi, wakati akizungumza mubashara katika kipindi cha Morning Trumpet kinachorushwa na Kituo cha Televisheni cha Azam TV, ambapo amefafanua hatua za kuomba leseni za madini pamoja na wajibu wa wamiliki wa leseni katika kuendeleza maeneo waliyopewa.

Akifafanua utaratibu wa kuomba leseni, Eng. Swedi amesema mwombaji anatakiwa kwanza kutambua eneo analokusudia kuwekeza na kuwasilisha maombi kupitia mfumo wa kielektroniki wa Mining Cadastre wa Tume ya Madini.

Amesema maombi hayo yanapaswa kuwasilishwa yakiwa na taarifa na nyaraka zinazohitajika kulingana na aina ya leseni inayoombwa. Aidha, Tume hufanya uhakiki wa eneo husika, uwezo wa kifedha na kitaalamu wa mwombaji pale inapohitajika, pamoja na kuzingatia vigezo vingine vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.

Akizungumzia usimamizi wa leseni, Eng. Swedi amesema Tume ya Madini inaendelea kufuatilia utekelezaji wa masharti ya leseni na maendeleo ya shughuli za uchimbaji katika maeneo husika ili kuhakikisha rasilimali za madini zinaendelezwa na kutumika kwa tija kwa manufaa ya wananchi na uchumi wa Taifa.

Amesisitiza kuwa Tume huchukua hatua za kisheria pale inapobainika kuwepo kwa ukiukwaji wa masharti ya leseni.

“Pale ambapo mmiliki atashindwa kurekebisha kasoro zilizobainika kwa mujibu wa utaratibu uliowekwa, Tume inaweza kuendelea na hatua za kusimamisha au kufuta leseni kwa mujibu wa sheria,” amesema Eng. Swedi.

Aidha, amewahimiza Watanzania, hususan wachimbaji wadogo na wawekezaji, kutumia fursa zilizopo katika sekta ya madini kwa kuzingatia taratibu rasmi na kutekeleza wajibu wao katika kuendeleza rasilimali hizo.

“Napenda kutumia nafasi hii kuwakumbusha wananchi kuwa sekta ya madini ina fursa nyingi za uwekezaji kwa Watanzania, wakiwemo wachimbaji wadogo. Tume ya Madini itaendelea kutoa elimu, kurahisisha upatikanaji wa leseni na kusimamia utekelezaji wa sheria ili kuhakikisha rasilimali za madini zinawanufaisha wananchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Eng. Swedi.