Na Mwandishi Wetu–Dar es Salaam
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amezihimiza Tume za Uchaguzi za Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuweka mikakati ya pamoja ya kukabiliana na taarifa za uongo na upotoshaji kuhusu chaguzi unaosambazwa kupitia mitandao ya kijamii, akisisitiza kuwa hatua hiyo ni muhimu katika kulinda uaminifu wa wananchi kwa mifumo ya uchaguzi, amani na utulivu katika ukanda huo.
Akizungumza Novemba 23, 2026, wakati wa Mkutano wa Jukwaa la Tume za Uchaguzi za Nchi za SADC (ECF-SADC), uliofanyika jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu amesema mitandao ya kijamii imekuwa na nafasi kubwa katika michakato ya uchaguzi kutokana na uwezo wake wa kusambaza taarifa kwa haraka, kutoa elimu ya mpiga kura, kutangaza uandikishaji na kuongeza ushiriki wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Amesema pamoja na fursa hizo, matumizi ya mitandao ya kijamii yameibua changamoto ya taarifa za uongo zinazoweza kupotosha wananchi, kuathiri taswira ya taasisi za uchaguzi na kusababisha migawanyiko katika jamii. Hivyo, amezitaka tume hizo kuimarisha mifumo ya mawasiliano na kuhakikisha zinatoa taarifa sahihi kwa wakati ili kuzuia mianya inayoweza kutumiwa kusambaza upotoshaji.
“Uwazi katika utoaji wa taarifa ni muhimu ili wananchi wanapokutana na taarifa zinazohusu uchaguzi waweze kupata taarifa sahihi, kwani taarifa zisizo sahihi zinazosambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii zinaweza kuleta athari hasi katika jamii na kuathiri mfumo wa uchaguzi,” amesema Waziri Mkuu.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa tume za uchaguzi kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto zinazotokana na maendeleo ya teknolojia, ikiwemo matumizi yanayoongezeka ya akili unde (AI). Ameeleza kuwa kipindi ambacho nchi hazipo kwenye uchaguzi kinapaswa kutumiwa na tume hizo kutafakari, kubadilishana uzoefu na kuandaa mikakati ya pamoja itakayoboresha usimamizi wa uchaguzi, huku wadau wote wakihimizwa kuheshimu sheria, taratibu na kanuni za uchaguzi.
Mkutano huo wenye kaulimbiu isemayo “Usimamizi wa uchaguzi na mitandao ya kijamii: Kubainisha wajibu wa Tume za Uchaguzi katika Ukanda wa Kusini mwa Afrika” unatoa fursa kwa tume hizo kujadili wajibu wake katika matumizi ya mitandao ya kijamii na kubadilishana uzoefu kuhusu usimamizi wa chaguzi.
Kwa upande wake, Rais wa Jukwaa la ECF-SADC na Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ya Angola, Jaji Dkt. Manuel Pereira da Silva, amesema jukwaa hilo limekuwa muhimu katika kujenga uwezo wa tume za uchaguzi kupitia kubadilishana uzoefu, kujifunza mbinu bora na kuendeleza mifumo huru na isiyoegemea upande wowote.
Ameongeza kuwa ushirikiano huo umechangia kuimarisha uwezo wa kitaasisi wa tume za uchaguzi na kujenga mazingira ya amani, utulivu na demokrasia katika nchi za Afrika, kupitia shughuli zikiwemo uangalizi wa uchaguzi na programu za kimataifa za kubadilishana uzoefu.
Naye Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi ya Tanzania, Jaji wa Rufaa, Mhe. Jacobs Mwambegele, amesema jukwaa la ECF-SADC limekuwa likitoa fursa kwa Tume za uchaguzi kujifunza na kubadilishana uzoefu katika masuala mbalimbali yanayohusiana na usimamizi na uendeshaji wa chaguzi.
“Aidha, limetusaidia katika kuimarisha mifumo ya uchaguzi na kutujengea uwezo zaidi katika kutekeleza majukumu yetu.” amesema Mhe. Jaji Mwambegele.
Amesisitiza kiwa Tume hiyo imekuwa ikishiriki katika shughuli mbalimbali za uchaguzi katika nchi wanachama wa jukwaa hilo, zikiwemo misheni za uandikishaji wapiga kura na usimamizi wa uchaguzi, hatua inayoiwezesha kupata uzoefu na kujifunza mbinu bora za kuimarisha usimamizi wa chaguzi.
“Jukwaa hili lina umuhimu na mchango mkubwa katika kuimarisha demokrasia na uchaguzi katika nchi za ukanda wa SADC. Kupitia ushiriki wetu, tumepata fursa ya kuona, kujifunza na kubadilishana uzoefu kuhusu masuala yanayohusiana na uendeshaji wa chaguzi zetu,” amesisitiza Jaji Mwambegele.
Ameongeza kuwa katika kipindi cha mkutano huo, wajumbe watajadili mada mbalimbali na kubadilishana uzoefu kuhusu utekelezaji wa majukumu yao ya kusimamia na kuratibu uchaguzi, pamoja na kupitia ajenda mbalimbali kwa mujibu wa taratibu za jukwaa hilo.

