Na Denis Mlowe 

MJUMBE wa Kamati Ndogo ya uhamasishaji vijana michezo utamaduni Sanaa wazazi CCM Taifa Joseph Mgongolwa kutoka Mkoa wa Iringa amempongeza Kamanda wa Polisi Mkoa wa Iringa, SACP Allan Bukumbi, kwa juhudi za kuimarisha usalama, kuboresha vitendea kazi vya jeshi la polisi, kurejesha nidhamu kwa askari na kupunguza matukio ya uhalifu mkoani humo.

Akizungumza na wanahabari mkoa wa Iringa Joseph Mgongolwa amesema wameona mabadiliko katika utendaji wa Jeshi la Polisi, akitaja ujenzi na uboreshaji wa vituo vya polisi, ukarabati wa magari yaliyokuwa yameharibika pamoja na kuhakikisha vituo vinakuwa na vitendea kazi vinavyorahisisha shughuli za ulinzi na usalama.

Mgongolwa amesema hatua hizo zimechangia kurejesha heshima ya jeshi hilo kwa wananchi, huku akieleza kuwa usimamizi wa Kamanda Bukumbi umeongeza nidhamu kwa askari na kuimarisha utendaji wa kazi zao.

Amesema wananchi wanapaswa kuendelea kuwa na imani na Jeshi la Polisi na kutoa ushirikiano katika kufichua vitendo vya uhalifu, akieleza kuwa usalama wa jamii unategemea pia ushirikiano wa wananchi na vyombo vya dola.

Mgongolwa ameeleza kuwa kampeni ya “Ongea na Kamanda” imekuwa na mchango mkubwa katika kuimarisha mawasiliano kati ya polisi na wananchi, kwa kuwa kamanda amekuwa akitembelea maeneo mbalimbali na kusikiliza changamoto zinazowakabili wananchi, hatua ambayo amesema imeongeza uelewa, uwazi na uaminifu katika ushirikiano wa pande hizo mbili.

Aidha, amesema kupitia kampeni hiyo na mikakati mingine ya kiusalama, matukio ya mauaji, ubakaji na uhalifu mwingine yamepungua kwa kiwango kikubwa, akidai baadhi ya matukio hayo yamepungua kwa takribani asilimia 90.

Katika pongezi hizo, Mgongolwa pia ameishukuru Serikali na uongozi wa Jeshi la Polisi kwa kuendelea kusimamia maboresho ya kiutendaji, huku akimpongeza Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, kwa ushirikiano wake katika masuala ya usalama na maendeleo ya mkoa.

Amesema Mkuu wa Mkoa Kheri James amekuwa akifanya kazi kwa karibu na vyombo vya usalama kutokana na nafasi yake ya kuongoza Kamati ya Usalama ya Mkoa, akieleza kuwa uongozi wake umechangia kuimarisha usimamizi wa masuala ya usalama.

Katika hatua nyingine, Mgongolwa ametoa ombi kwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) kumwangalia SACP Bukumbi kwa uwezekano wa kuongezewa muda wa utumishi endapo atakuwa karibu na kustaafu, akieleza kuwa wanaamini kuendelea kwa uongozi wake kutasaidia kudumisha mafanikio yaliyopatikana katika kuimarisha usalama wa Iringa.

Amesema ombi hilo linatokana na mabadiliko yaliyofanywa na kamanda huyo katika kuboresha utendaji wa jeshi, kuimarisha nidhamu, kufufua magari ya polisi na kuongeza ushirikiano kati ya wananchi na polisi.

Kwa upande wake, Maximilian Lugenge amesisitiza umuhimu wa wananchi kuendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa vyombo vya usalama na kushiriki kikamilifu katika polisi jamii, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuzuia uhalifu na kujenga jamii yenye amani.