
Na Farida Mangube Morogoro
Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Ali Kakurwa, ameitaka Menejimenti ya Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA), kwa kushirikiana na madaktari wa mifugo nchini, kuimarisha juhudi za kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ili kulinda afya za wanyama na binadamu.
Dkt. Bashiru ametoa agizo hilo wakati wa uzinduzi wa mbio za hisani zilizofanyika katika kuadhimisha miaka 50 tangu kuanzishwa kwa mafunzo ya udaktari wa mifugo nchini Tanzania katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) mwaka 1976. Mbio hizo zilihusisha kilomita 21.1, kilomita 10 na kilomita tano, ambapo Waziri huyo pia alishiriki mbio za kilomita tano.
Akizungumza baada ya kuzindua mbio hizo, Dkt. Bashiru amesema kuwa SUA, kwa kushirikiana na madaktari wa mifugo nchini, ina uwezo wa kuweka mikakati madhubuti ya kudhibiti na hatimaye kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa ndani ya miaka 20 ijayo, kupitia udhibiti wa maambukizi kwa mbwa, paka na wanyama wengine wanaoweza kusambaza ugonjwa huo.
Amesisitiza kuwa masuala ya afya ya mifugo, yakiwemo chanjo, tiba, usajili na utambuzi wa magonjwa, yanapaswa kupewa kipaumbele ili kufanikisha kampeni ya kutokomeza ugonjwa huo.
“Afya ya mifugo kwa upana wake, chanjo, tiba, usajili na utambuzi wa magonjwa kwa mifugo viwe kipaumbele. Hakuna atakayeendesha kampeni ya kutokomeza ugonjwa wa kichaa cha mbwa kama si chuo hiki na madaktari waliozalishwa hapa,” amesema Dkt. Bashiru.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuweka mifumo bora ya utunzaji na uhifadhi wa wanyama, ikiwemo kuwapatia matibabu wanapougua, ili kuhakikisha wanaishi katika mazingira salama na yasiyohatarisha afya za binadamu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Ndaki ya Tiba ya Wanyama na Sayansi za Afya ya SUA, Profesa Esron Karimuribo, amesema kuwa maadhimisho hayo yanalenga kutambua na kuenzi mchango wa SUA pamoja na wataalamu wake katika maendeleo ya tiba ya wanyama na sekta ya mifugo nchini.
Amesema chuo hicho kimekuwa na mchango mkubwa katika kuzalisha madaktari wa mifugo na wataalamu wa afya ya wanyama ambao wameendelea kusaidia kujenga jamii yenye ustawi na afya bora ya wanyama na mifugo.
Profesa Karimuribo ameongeza kuwa mbio hizo pia zililenga kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kufanya mazoezi ili kuimarisha afya na kupunguza hatari ya magonjwa yasiyoambukiza.
“Mkusanyiko huu utasaidia kuimarisha mshikamano na ustawi wa jamii, kupunguza msongo wa mawazo na kuimarisha afya za watumishi wa chuo, wanafunzi pamoja na jamii ya Watanzania kwa ujumla,” amesema.
Baadhi ya washiriki wa mbio hizo, akiwemo mshindi wa kwanza wa mbio za kilomita 21.1, Doricas Bonifasi kutoka mkoani Arusha, pamoja na Kessy Kombo, ambaye ana ulemavu wa miguu na kushiriki mbio za kilomita tano, wamesema kuwa maadhimisho hayo yamewakutanisha wadau wengi wa michezo kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Wamesema kuwa ushiriki wao katika mbio hizo unachangia kuimarisha afya zao, kuongeza mshikamano na kujenga umoja miongoni mwa Watanzania, hususan wadau wa riadha.
Jumla ya washiriki 546, wakiwemo watumishi wa SUA na familia zao, wanafunzi pamoja na wadau kutoka mikoa mbalimbali nchini, walishiriki katika mbio hizo zilizoongozwa na Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Bashiru Ali Kakurwa.
Maadhimisho ya miaka 50 tangu kuanzishwa kwa mafunzo ya udaktari wa mifugo nchini katika Chuo Kikuu cha Sokoine cha Kilimo (SUA) yalidhaminiwa na Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO).
