* Asema Serikali imeboresha utaratibu wa upatikanaji wa fedha za miradi ya barabara
*Atarejea kukagua maendeleo ya ujenzi
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amemtaka mkandarasi anayejenga sehemu ya barabara ya Bigwa–Mvuha–Kisaki, yenye urefu wa jumla wa kilomita 133, mkoani Morogoro, aongeze kasi ya ujenzi kwa kuhakikisha mitambo na wataalamu wanaohitajika wanafika eneo la mradi.
Dkt. Mwigulu ametoa agizo hilo leo, (Jumapili, Novemba 22, 2026), wakati akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Kata ya Bwakila Chini, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, mkoani Morogoro.
Amesema amepita katika barabara hiyo na kujionea hali yake, huku akieleza kuwa ziara yake imelenga kuongeza msukumo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
“Kuona kwenye makaratasi ni tofauti na kuona kwa macho. Kuona kwenye taarifa ni tofauti na kuona saiti kama leo ambavyo nimeiona mwenyewe barabara hii,” amesema.
Waziri Mkuu amekiri kuwa ujenzi wa barabara hiyo umechelewa, lakini ameeleza kuwa ucheleweshaji huo haukutokana na uzembe wa ufuatiliaji wa wabunge au viongozi wa mkoa.
Amesema Serikali ilifanya uamuzi wa kimkakati wa kuelekeza fedha katika kukamilisha Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere ili kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa umeme nchini.
Hata hivyo, Waziri Mkuu amesema tangu kuanza kwa mwaka wa fedha wa 2026/2027, Serikali imebadilisha utaratibu wa upatikanaji wa fedha za miradi ya barabara kwa kuzielekeza moja kwa moja katika Mfuko wa Barabara, ambao unapokea zaidi ya Sh. bilioni 330 kila mwezi.
“Maana yake, kuanzia sasa na huko tunakokwenda, hapatakuwepo na kisingizio cha ucheleweshaji wa fedha kwenye utekelezaji wa barabara yenu hii,” amesema.
Amemtaka mkandarasi kuongeza mitambo na wataalamu katika eneo la mradi badala ya kuwa na watumishi wachache wanaolinda kambi, huku akisisitiza kuwa atafuatilia kwa karibu maendeleo ya ujenzi.
“Na mimi nitaifuatilia kweli kweli barabara hii, kwa sababu nimepita nimeiona,” amesema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu barabara hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Mhandisi Godfrey Kasekenya, amesema hatua ya kwanza ya mradi huo inahusisha ujenzi wa kilomita 78 kutoka Bigwa hadi Mvuha.
Amesema kuchelewa kwa malipo ya awali kumeathiri kasi ya utekelezaji wa mradi, lakini Wizara ya Ujenzi inatarajia kukamilisha malipo hayo wiki inayofuata ili mkandarasi aweze kuongeza kasi ya kazi.
Awali, Mbunge wa Morogoro Kusini Mashariki, Hamisi Taletale, akizungumza pia kwa niaba ya Mbunge wa Morogoro Kusini, Zuberi Mfaume, alimweleza Waziri Mkuu kuwa kuchelewa kwa ujenzi wa barabara hiyo kumekuwa changamoto kwa wananchi.
Amesema mkandarasi amelipwa Sh. bilioni 9 lakini bado anadai takribani Sh. bilioni 6, huku akiiomba Serikali kuhakikisha malipo yaliyobaki yanafanyika mapema ili kuongeza kasi ya ujenzi.

