Na Mwamvua Mwinyi, Pwani

Novemba 22, 2026

WAZIRI Mkuu Dkt. Mwigulu Nchemba amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ameweka rekodi katika kuimarisha sekta ya afya nchini kwa kujenga zahanati 2,700, vituo vya afya 600, hospitali za wilaya 119 pamoja na kutoa magari ya huduma za afya kwa kila mkoa.

Aidha, katika sekta ya elimu, amesema Serikali imejenga shule za msingi 2,700 na shule za sekondari 1,300, huku kila mkoa ukiwa na shule za wasichana, pamoja na kujenga shule 29 za ufundi na shule 100 za amali.

Akizungumza Novemba 21, 2026, wakati akihitimisha ziara yake ya kikazi mkoani Pwani, Dkt. Mwigulu amesema Rais Samia ameonyesha dhamira na jitihada kubwa katika uwajibikaji na kuboresha huduma kwa wananchi, hivyo viongozi na watendaji wanapaswa kutekeleza maelekezo ya Serikali kwa uaminifu bila kufifisha juhudi hizo.

“Serikali imejenga hospitali, vituo vya afya, imeweka dawa, unakuta watu wanazuiliwa miili ya marehemu wao, hospitali zinazuia miili ya marehemu, ziache mambo hayo,” amesema.

Vilevile, amekemea tabia ya baadhi ya hospitali kuwatoza ndugu wa wagonjwa wa dharura fedha za mafuta ya magari ya wagonjwa (ambulance), pamoja na kuwaamuru wanawake wajawazito wanaofika kujifungua kuleta vifaa kama ndoo na beseni, akisisitiza kuwa vitendo hivyo havipaswi kuendelea.

Dkt. Mwigulu amewaonya watendaji wazembe wanaojificha nyuma ya viongozi na watendaji wengine wanaowajibika, akitaka kila mmoja kutekeleza majukumu yake kwa kufuata sheria, taratibu na maelekezo ya Serikali, huku akisisitiza wanaokiuka wafukuzwe kazi ili iwe fundisho kwa wengine.