Happy Lazaro ,Dar es Salaam.
Dar es Saalam .MCHIMBAJI wa dhahabu kutoka mkoani Geita, Omary Kamage, ameiomba Serikali na wadau wa sekta ya madini kuongeza fursa za kuwawezesha wachimbaji wadogo kupata mitaji na teknolojia za kisasa zitakazowasaidia kuongeza uzalishaji na kukuza biashara zao.
Kamage, ambaye ni mmiliki wa kampuni ya Kamage Investments, alisema changamoto ya upatikanaji wa fedha na vifaa vya kisasa bado ni kikwazo kwa baadhi ya wachimbaji wadogo wenye nia ya kupanua shughuli zao na kuingia katika uchimbaji wa kiwango cha kati.
Amesema ameshiriki maonesho ya madini jijini Dar es Salaam kwa lengo la kutafuta maarifa mapya, kujifunza mbinu za kisasa za uchimbaji pamoja na kukutana na kampuni zinazoweza kushirikiana naye katika kukuza uwekezaji wake.
Aidha ameongeza kuwa kupitia maonesho hayo amepata nafasi ya kuzungumza na wawekezaji mbalimbali ambao wameonesha utayari wa kujadili uwezekano wa kutoa mitaji kwa kampuni yake ili iweze kuongeza uwezo wa uzalishaji.
Kamage amefafanua moja ya maeneo anayoyapa kipaumbele ni kujifunza teknolojia za uchimbaji na uchakataji wa madini, ikiwemo mfumo wa CIP, ambao anaamini utawasaidia kupata ufanisi zaidi katika shughuli zao wanapopanua uwekezaji.
Amesema wachimbaji wadogo wanapaswa kuwa tayari kujifunza na kutumia fursa zinazopatikana nje ya maeneo yao ya kazi, kwa kuwa maendeleo ya biashara ya madini yanahitaji maarifa, ubunifu na kujenga ushirikiano na wadau mbalimbali.
Hata hivyo amepongeza Wizara ya Madini inayoongozwa na Waziri Anthony Mavunde kwa kutoa nafasi kwa wachimbaji wadogo kushiriki maonesho hayo, akisema hatua hiyo inawapa nafasi ya kutangaza shughuli zao na kuunganishwa na wadau wenye uwezo wa kuwekeza.
Akizungumzia vijana wanaotamani kujihusisha na shughuli za uchimbaji na biashara, Kamage aliwataka kuwa na uvumilivu, nidhamu na moyo wa kujituma, akisisitiza kuwa mafanikio yanahitaji kuanza na hatua ndogo na kuendelea kupambana licha ya changamoto.
Aidha ameongeza pia wanatarajia kupata nafasi ya kuwasilisha maoni yao kwa Serikali, ikiwemo kuomba kukutana na Rais Samia Suluhu Hassan, ili kueleza changamoto na mahitaji ya wachimbaji wadogo kwa lengo la kuboresha mazingira ya uwekezaji katika sekta hiyo.
