Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki anayeshughulikia masuala ya Afrika Mashariki, Mhe. James Kinyasi Millya (Mb.), amewasili jijini Addis Ababa, Ethiopia, kuongoza ujumbe wa Tanzania katika maandalizi na ushiriki wa nchi katika Mkutano wa Tano wa Kimataifa kuhusu Afya ya Umma Afrika (Fifth International Conference on Public Health in Africa – CPHIA 2026).
Mhe. Millya amewasili jijini humo tarehe 21 Novemba 2026 kupitia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Addis Ababa Bole, akiambatana na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Balozi Said Shaib Mussa. Viongozi hao wamepokelewa na Balozi wa Tanzania nchini Ethiopia na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Afrika (AU) na Tume ya Umoja wa Mataifa ya Uchumi Afrika (UNECA), Mhe. Innocent Eugene Shio.
Baada ya kuwasili, Mhe. Millya na ujumbe wake walifanya kikao cha ndani cha maandalizi ya ushiriki wa Tanzania katika mkutano huo, unaotarajiwa kufanyika kwa siku tatu kuanzia tarehe 22 hadi 24 Novemba 2026, na kushirikisha Wakuu wa Nchi na Serikali, viongozi wa taasisi za kikanda na kimataifa pamoja na wadau mbalimbali wa sekta ya afya barani Afrika.
Aidha, mkutano huo utakuwa jukwaa muhimu la kujadili masuala mbalimbali yanayohusu afya ya umma barani Afrika, ikiwemo kuimarisha mifumo ya afya, kuboresha upatikanaji wa huduma bora za afya na kuimarisha ushirikiano wa nchi za Afrika katika kukabiliana na changamoto za sekta ya afya kwa manufaa ya wananchi wa bara hilo.
Viongozi wengine walioshiriki kikao hicho ni pamoja na Mshauri wa Rais anayeshughulikia Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto Bi. Ummy Mwalimu.

