Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Ngwaru Jumanne Maghembe (Mb.), ameiwakilisha Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano wa Sita wa Jukwaa la Aswan kuhusu Amani na Maendeleo Endelevu, unaofanyika jijini Aswan nchini Misri, kuanzia Novemba 21 hadi 22, 2026.

Mkutano huo umewakutanisha viongozi wa Serikali,Mashirika ya Kimataifa, watunga sera na wataalamu wa Usalama, kutoka Afrika na maeneo mbalimbali duniani kwa lengo la kujadili namna ya kujenga amani endelevu, usalama na maendeleo endelevu barani Afrika. 

Katika ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Novemba 21, 2026, washiriki walijadiliana kuhusu nafasi ya Afrika kushiriki kikamilifu kwenye maamuzi na mifumo ya kimataifa katika kipindi cha mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kiteknolojia duniani.

Vilevile, Majadiliano hayo yamejikita katika kutafuta suluhu za pamoja kuhusu changamoto zinazoikabili Afrika, ikiwemo usalama wa chakula, migogoro, ufadhili wa maendeleo, mabadiliko ya tabianchi na matumizi ya teknolojia mpya, hususan akili unde (AI), kwa manufaa ya wananchi. 

Aidha, washiriki walijadili kwa kina kuhusu sauti na maslahi ya Afrika yanavyopaswa kuzingatiwa katika maamuzi ya kimataifa.

Ushiriki wa Tanzania katika jukwaa hilo unaonesha dhamira ya Serikali ya kuimarisha Diplomasia, kudumisha amani na kukuza ushirikiano wa kikanda na kimataifa. Aidha, unatoa fursa kwa Tanzania kuendeleza ushirikiano wa kiuchumi, usalama na maendeleo ya pamoja, huku ikiendelea kuchangia juhudi za kutafuta amani na utulivu barani Afrika.

Mkutano huo unatarajiwa kuhitimishwa kwa kupitishwa kwa maazimio yatakayojulikana kama “Aswan Conclusions,” yatakayotoa mwongozo wa utekelezaji wa masuala yaliyojadiliwa. Kupitia ushiriki huo, Tanzania inalenga kuimarisha nafasi yake katika diplomasia ya kimataifa na kuhakikisha maslahi ya taifa pamoja na ya Afrika yanapewa kipaumbele.