WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amesisitiza kuwa hukumu za mahakama lazima ziheshimiwe na kutekelezwa kwa mujibu wa sheria, akisema mtu asiyeridhika na uamuzi wa mahakama anapaswa kutumia taratibu za kisheria kuupinga badala ya kuzuia utekelezaji wake.
Ameyasema hayo leo, Jumamosi, Novemba 21, 2026, wakati akizungumza na wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya Shule ya Msingi Mtongani, Halmashauri ya Wilaya ya Kibaha, mkoani Pwani.
Kauli hiyo imefuatia malalamiko ya Omari Rajabu Mganga, mkazi wa Kata ya Janga, aliyedai kushinda kesi ya ardhi katika Mahakama Kuu lakini bado anakabiliwa na mgogoro baada ya eneo hilo kudaiwa kuuzwa kwa mtu mwingine.
“Maelekezo ya mahakama hayawezi kupindishwa pindishwa kwa njia isiyo ya kisheria,” amesema Dkt. Mwigulu.
Ameelekeza afisa wa sheria na Jeshi la Polisi kuhakiki nyaraka za kesi hiyo na, iwapo hukumu itathibitisha madai ya mlalamikaji, kushirikiana na Mkuu wa Wilaya kuhakikisha anakabidhiwa eneo hilo kwa mujibu wa sheria.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka vipaumbele vitatu vya kuharakisha utekelezaji wa miradi ya barabara nchini, ambavyo ni kurejesha kasi ya miradi iliyokwama kutokana na changamoto za malipo, kutoa fedha za awali kwa wakandarasi wenye mikataba na kukamilisha taratibu za miradi ambayo wakandarasi wamepatikana lakini mikataba haijasainiwa.
Amesema zaidi ya Sh. bilioni 330 zimepelekwa kwenye mifuko ya barabara katika kipindi cha takribani mwezi mmoja, kufuatia utaratibu wa kuelekeza fedha moja kwa moja kwenye mifuko hiyo ili kuharakisha utekelezaji wa miradi.
Aidha, ameelekeza mkandarasi wa barabara ya Mlandizi–Stesheni ya SGR (Ruvu), yenye urefu wa kilometa 23, kulipwa fedha za awali ili kuharakisha kuanza kwa ujenzi, huku akizitaka mamlaka husika kukamilisha masuala ya uthamini na fidia ili kuondoa vikwazo vya utekelezaji wa mradi huo.