Meneja uendelezaji biashara ya baruti kutoka kampuni hiyo,Rayson Nkya akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam kuhusu huduma zinazotolewa na kampuni hiyo

…………

Happy Lazaro, Dar es Salaam.

Dar es Saalam.Kampuni ya uuzaji na usambazaji wa chemikali na baruti Tanzania ETG CURECHEM Ltd imesisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa maonesho ya sekta ya madini mara kwa mara, ikieleza kuwa majukwaa hayo yanatoa fursa kwa kampuni, wawekezaji na wadau mbalimbali kukutana, kujadili changamoto na kutafuta njia za kuboresha shughuli zao.

Akizungumza katika maonesho ya madini na uwekezaji yanayoendelea jijini Dar es Saalam ,Meneja uendelezaji biashara ya baruti kutoka kampuni hiyo,Rayson Nkya amesema ushiriki wao unalenga kuimarisha mahusiano na wateja waliopo, kutafuta wateja wapya na kuwafikia wawekezaji wanaohitaji huduma za kampuni hiyo.

Amesema kampuni hiyo inayojihusisha na usambazaji wa kemikali na baruti kwa shughuli za uchimbaji madini ina makao makuu Dar es Salaam na matawi Kahama, Geita na Lugoba, ambako pia kuna maghala maalumu ya kuhifadhi baruti kwa kuzingatia taratibu zinazotakiwa.

Nkya amesema kuwa kampuni hiyo husambaza baruti za kibiashara (Commercial Explosives) zinazotumika kulipua miamba katika machimbo ya kokoto na maeneo ya uchimbaji wa madini mbalimbali yakiwemo dhahabu, shaba na madini mengine ya metali, huku ikizingatia ubora wa bidhaa, bei nafuu na uwasilishaji wa haraka.

Amesema mbali na kusambaza bidhaa hizo, kampuni pia hutoa elimu kwa wateja kuhusu sheria na taratibu za matumizi, usafirishaji na uhifadhi wa baruti pamoja na msaada wa kitaalamu ili kuhakikisha shughuli za uchimbaji zinafanyika kwa kuzingatia usalama na matakwa ya kisheria.

“Maonesho hayo pia yamekuwa fursa ya kukutana na mamlaka zinazohusika na usimamizi wa sekta ya kemikali na baruti, jambo linalorahisisha mawasiliano na majadiliano ya kina kuhusu masuala mbalimbali ambayo wakati mwingine ni vigumu kuyajadili kutokana na majukumu na ratiba za kila siku.”amesema Nkya .

Ameongeza kuwa jukwaa hilo halina manufaa kwa kampuni zinazofanya biashara pekee, bali hata washindani wao wanapata nafasi ya kukutana, kubadilishana uzoefu na kujadili changamoto zinazokabili sekta, hatua inayoweza kusaidia kutafuta suluhisho la pamoja na kuboresha mazingira ya biashara.

Aidha, amewaalika wadau wa madini na wawekezaji kutembelea banda la kampuni hiyo katika maonesho hayo kwa ajili ya kupata maelezo ya bidhaa na huduma kutoka kwa wataalamu wa kemikali, baruti na masoko, huku akihimiza maonesho hayo yaendelea kufanyika mara kwa mara kutokana na mchango wake katika kujenga ushirikiano na kukuza sekta ya madini nchini.