Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Rodgers Elisha Nelson akizungumza kwenye maonesho hayo jijini Dar Es Salaam 

Happy Lazaro, Dar es Saalam

Dar es Saalam.KAMPUNI ya Permanent Minerals inayojihusisha na uchimbaji wa madini ya Graphite imesema maonesho ya kimataifa ya madini yamekuwa fursa muhimu ya kutangaza bidhaa zake na kuunganisha kampuni hiyo na wanunuzi wa ndani na nje ya nchi.

Akizungumza katika maonesho hayo Msaidizi wa Mkurugenzi Mkuu wa kampuni hiyo, Rodgers Elisha Nelson, amesema ushiriki wao umewawezesha kukutana na wadau mbalimbali wanaohitaji madini ya Graphite na ambao awali hawakuwa na taarifa sahihi za mahali yanapopatikana.

Amesema kampuni hiyo imekuwa ikijikita katika uchimbaji wa Graphite, ambayo ni miongoni mwa madini yenye matumizi muhimu katika viwanda mbalimbali na yanayoendelea kupata uhitaji mkubwa kutokana na fursa za kiuchumi zinazotokana na matumizi yake.

“Pamoja na Mererani kufahamika zaidi kwa uzalishaji wa Tanzanite, eneo hilo pia lina utajiri wa Graphite ambao unapaswa kutangazwa zaidi ili kuongeza mchango wake katika uchumi na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika soko la madini.”amesema Rodgers.

Amefafanua kuwa kupitia maonesho hayo wamekutana na wadau wa madini mbalimbali yakiwemo dhahabu, Tanzanite na Copper, pamoja na washiriki wa kimataifa waliokuwa wakitafuta Graphite, jambo lililowapa nafasi ya kujenga mahusiano mapya ya kibiashara.

“Kampuni hiyo pia imekuwa ikinufaika na ushirikiano wa Serikali kupitia utoaji wa vibali vya kusafirisha madini, usimamizi wa shughuli za uchimbaji na msaada wa kitaalamu kutoka kwa maafisa wanaohusika na sekta hiyo.”amesema Rodgers. 

Ameongeza kuwa maonesho hayo yamechangia kufungua fursa za masoko mapya kwa kuwawezesha wazalishaji kukutana moja kwa moja na wanunuzi, huku akisisitiza umuhimu wa Serikali kuendelea kuwaunga mkono wachimbaji na wafanyabiashara wa madini kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji.

Aidha amewataka wawekezaji na wanunuzi wanaohitaji madini ya Graphite kushirikiana na Permanent Minerals, inayopatikana Milima Mitatu, Mererani, Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, ili kutumia fursa zilizopo katika biashara ya madini hayo.