Meneja Masoko Mwandamizi wa kampuni hiyo,Godfrey Reuben akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Saalam katika.maonesho hayo

Happy Lazaro, Dar es Salaam

Dar es Saalam. KAMPUNI ya Superdoll inayojihusisha na usambazaji wa matairi makubwa ya mitambo ya uchimbaji wa madini imeiomba Serikali kuendeleza maonesho na majukwaa ya biashara ya madini katika mikoa mbalimbali nchini ili kuwafikia wadau wengi zaidi na kuongeza fursa za kibiashara.

Akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya Madini yanayoendelea jijini Dar es Salaam ,Meneja Masoko Mwandamizi wa kampuni hiyo,Godfrey Reuben amesema maonesho ya mwaka huu yamekuwa na tofauti kubwa kutokana na kushiriki kwa wawakilishi wengi wa kampuni mbalimbali wenye mamlaka ya kufanya maamuzi, jambo linaloongeza uwezekano wa kupata washirika na wateja wapya.

Amesema kuwa,kampuni hiyo imekuwa ikishiriki maonesho ya aina hiyo kwa mara ya tano au sita, huku mwaka huu ikiwa na furaha kutokana na mwitikio wa wadau na fursa za kukutana moja kwa moja na watu wanaohusika na maamuzi ya ununuzi wa vifaa katika kampuni za madini.

“Kampuni hiyo inasambaza matairi makubwa yanayotumika kwenye mitambo ya migodini pamoja na vipuri mbalimbali vinavyohusiana na shughuli za uchimbaji, bidhaa ambazo zina manufaa kwa wachimbaji wadogo, wa kati na wakubwa.”amesema Godfrey .

Ameongeza kuwa, katika maonesho hayo wameshiriki kwa kushirikiana na kampuni kutoka China inayozalisha matairi, ambapo ushirikiano huo unalenga kuleta bidhaa zitakazosaidia kuongeza ufanisi na tija katika shughuli za uchimbaji wa madini.

Aidha aliitaka Serikali kupeleka maonesho hayo katika mikoa mingine yenye shughuli nyingi za uchimbaji, hususani Kanda ya Ziwa na mikoa ya Kusini, akieleza kuwa kufanya hivyo kutawawezesha wadau ambao hawana nafasi ya kufika Dar es Salaam kushiriki na kutafuta fursa za kibiashara.

Godfrey amesema kuwa, kampuni hiyo yenye makao makuu Dar es Salaam ina matawi katika mikoa ya Mwanza, Arusha na Dodoma, huku ikiwa na mawakala na wasambazaji katika maeneo mengine ikiwemo Kusini na Songea, hatua inayorahisisha upatikanaji wa bidhaa zake kwa wateja wa maeneo mbalimbali.

“Naomba nitumie fursa hii kuwakaribisha wachimbaji na wadau wa sekta ya madini kutembelea matawi ya kampuni hiyo na kupata huduma za matairi pamoja na vipuri vya mitambo ya migodini, akisisitiza kuwa kampuni inaendelea kupanua mtandao wake wa huduma ili kuwafikia wateja wengi zaidi nchini.”amesema Godfrey.