* Mafunzo yalilenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na ufanisi wa Menejimenti ya REA.

* Mha. Saidy awataka viongozi kuzingatia maadili na taratibu za kiitifaki.

Dar es Salaam

Mwanadiplomasia mwandamizi, Balozi Omar Kashera Mjenga, ndc, amewajengea uwezo wajumbe wa Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kuhusu itifaki na maadili ya kiuongozi.

Mafunzo hayo yalilenga kuimarisha weledi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya viongozi.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mha. Hassan Saidy, amewataka viongozi kuzingatia maadili ya utumishi wa umma na taratibu za kiitifaki.

Amesema misingi hiyo ni muhimu katika mawasiliano rasmi, mahusiano ya kikazi na ushirikiano na wadau wa maendeleo.

Mha. Saidy ameongeza kuwa uzingatiaji wa itifaki huimarisha nidhamu na kujenga taswira nzuri ya REA.

Kwa upande wake, Balozi Mjenga ameeleza misingi ya itifaki, mawasiliano rasmi na mwenendo unaofaa kwa viongozi.

Amesisitiza umuhimu wa kulinda heshima na hadhi ya Taasisi katika utekelezaji wa majukumu ya kiuongozi.

Aidha, Afisa TEHAMA kutoka Mamlaka ya Serikali Mtandao (eGA), Franco Haule, ametoa mafunzo kwa Menejimenti ya REA kuhusu usimamizi wa vikao kupitia mfumo wa eBoard.

Mafunzo hayo yamelenga kuwawezesha viongozi kutumia mfumo huo katika kuandaa, kusimamia na kufuatilia vikao kwa ufanisi, pamoja na kurahisisha upatikanaji na usimamizi wa nyaraka za vikao kwa njia ya kidijitali.

Mafunzo hayo ni sehemu ya jitihada za REA za kuimarisha uwezo wa Menejimenti, kuongeza ufanisi katika usimamizi wa vikao na kuboresha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika utekelezaji wa majukumu ya Taasisi.

Jitihada hizo pia zinalenga kuongeza ufanisi katika usimamizi wa miradi ya nishati vijijini na kuboresha huduma za nishati zinazotolewa kwa wananchi.