Morogoro, Novemba 18, 2026.

Tume ya Ushindani (FCC) inaendelea na utekelezaji wa mradi wa uandaaji wa mfumo wa kisasa wa kidijitali wa utendaji kazi wa Taasisi (FCC Automation), unaolenga kuboresha ufanisi wa kiutendaji, kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza tija katika utoaji wa huduma kwa Umma na wadau wake.

Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani (FCC), Bi. Khadija Ngasongwa, alipofanya ziara ya kutembelea na kukagua maendeleo ya mradi huo tarehe 18 Novemba 2026, katika kikao kazi cha majaribio na mapitio ya mfumo (FIMS UAT Workshop) kinachofanyika katika Hoteli ya Nashera, mkoani Morogoro.

Katika ziara hiyo, Bi. Ngasongwa alipata fursa ya kupatiwa maelezo na wataalam kuhusu hatua mbalimbali zilizofikiwa katika uandaaji wa mfumo huo, hususan maendeleo ya kiufundi, utendaji na ufanisi wa mfumo, kupitia ushirikiano wa watumishi wa FCC kutoka Kurugenzi na Idara mbalimbali za Taasisi, pamoja na wataalam na wakandarasi wanaosimamia utekelezaji wa mradi kutoka ICTPACK, ICT FCC na TMA.

Mradi huo ulioanza kuandaliwa takribani miaka miwili iliyopita, unatarajiwa kukamilika mwezi Juni 2027. Mfumo huo unaotumia teknolojia ya mtandao (Web-based System) utawezesha FCC kuboresha mifumo yake ya ndani ya kiutendaji sambamba na kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa Umma na wadau mbalimbali wa Taasisi.

Kupitia mfumo huo, wadau na wananchi wataweza kupata huduma za FCC kwa njia ya kielektroniki, ikiwemo usajili, kuwasilisha maombi ya huduma mbalimbali na kupata huduma zinazohusiana na shughuli za makampuni, kama vile uunganishaji wa miamala ya makampuni, ongezeko la mitaji na huduma nyingine zilizo chini ya mamlaka ya Tume. Hali hiyo itapunguza utegemezi wa taratibu za kawaida za ana kwa ana na kuwawezesha wadau kupata huduma kwa urahisi zaidi.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo, Bi. Ngasongwa alieleza kuwa kukamilika kwa mfumo huo kutaiwezesha FCC kuwa na nyenzo madhubuti za kiteknolojia zitakazoongeza ufanisi wa kazi, kuimarisha usimamizi wa shughuli za Taasisi na kuboresha utoaji wa huduma kwa Umma.

Alisisitiza kuwa mara baada ya mfumo kukamilika na kuandaliwa kikamilifu kwa matumizi ya watumishi wa FCC, Taasisi itatoa mafunzo kwa watumishi ili kuhakikisha wanakuwa na uelewa na uwezo wa kuutumia ipasavyo. Aidha, wadau wa FCC nao watapatiwa elimu na mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo huo ili waweze kunufaika na huduma zitakazotolewa kupitia mfumo huo wa kidijitali.

Vilevile, alibainisha kuwa utekelezaji wa mradi huo unaendana na maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, pamoja na maelekezo ya Wizara ya Viwanda na Biashara, yanayozitaka Taasisi za Umma kuimarisha matumizi ya mifumo ya TEHAMA inayoweza kuwasiliana na kubadilishana taarifa (interoperability), kwa lengo la kuongeza ufanisi na kuleta tija katika utoaji wa huduma kwa wananchi.

Kwa upande wa manufaa ya mfumo huo, kukamilika kwake kunatarajiwa kuleta maboresho makubwa kwa FCC na wadau wake kupitia kupunguza muda na gharama za upatikanaji wa huduma, kurahisisha uchakataji wa maombi, kuimarisha usahihi na usalama wa taarifa, kuwezesha ufuatiliaji wa maombi na miamala, pamoja na kuongeza uwazi na uwajibikaji katika utendaji kazi wa Taasisi.

Aidha, mfumo huo utaiwezesha FCC kuboresha uratibu wa shughuli zake kati ya Kurugenzi na Idara mbalimbali, kurahisisha upatikanaji na matumizi ya taarifa kwa ajili ya kufanya maamuzi, kuongeza tija kwa watumishi na kuimarisha usimamizi wa shughuli zinazohusu utekelezaji wa majukumu ya Tume.

Kikao kazi hicho cha FIMS UAT ni sehemu muhimu ya mchakato wa kuhakikisha mfumo unakidhi mahitaji ya kiutendaji ya FCC na watumiaji wake kabla ya kukamilika na kuanza kutumika rasmi. Ushirikiano kati ya wataalam wa TEHAMA, wakandarasi na watumishi wa FCC ni sehemu ya msingi katika kuhakikisha mfumo unaandaliwa kwa kuzingatia mahitaji halisi ya Taasisi na wadau wake.

Kupitia mradi huo, FCC inalenga kuimarisha matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake, kuendana na mwelekeo wa Serikali wa kujenga utumishi wa Umma unaotumia mifumo ya kisasa, inayounganishwa na kutoa huduma bora, zenye ufanisi na zinazomweka mwananchi mbele. pp