Na Hellen Mtereko,
Mwanza
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) imeziagiza halmashauri zote nchini kufanya tathmini ya kina na kuandaa maoteo ya wanafunzi wanaotarajiwa kujiunga na kidato cha kwanza Januari, 2028.
Akifunga mkutano mkuu wa 40 wa Jumuiya ya Tawala za Mitaa Tanzania (ALAT) Novemba 18, 2026 Mwanza, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI), Dkt. Festo Dugange, alisema hatua hiyo inatokana na utekelezaji wa Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ambapo Sera hiyo inaweka ukomo wa elimu ya msingi kuwa darasa la sita, hali itakayosababisha wanafunzi zaidi ya milioni 3 kuingia sekondari kwa mkupuo mmoja.
Dkt. Dugange ameelekeza suala la maoteo liwe ajenda ya kudumu katika vikao vya halmashauri ili kubaini mahitaji halisi ya miundombinu.
“Halmashauri zibaini idadi ya shule na vyumba vya madarasa vinavyohitajika kwaajili ya kuwapokea wanafunzi hao, pamoja na kiwango halisi cha upungufu wa miundombinu kilichopo ili kuanza kuchukua hatua za mapema,” alisema Dkt. Dugange.
Aliongeza kuwa Serikali imejipanga kushirikiana na mamlaka hizo kuboresha na kujenga madarasa mapya kabla ya Januari 2028 ili kuhakikisha hakuna mwanafunzi atakayekosa nafasi ya kusoma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini, amezitaka halmashauri kuongeza ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato na kuwa na watumishi wenye weledi ili kuondokana na utegemezi wa kibajeti.
Aidha, alishauri kuanzishwa kwa mashamba darasa ya mazao kama kahawa ili kutoa elimu kwa vitendo kwa wakulima. Vilevile, alisisitiza kudumisha mahusiano mazuri kazini, kuhakikisha ulinzi na usalama, pamoja na kuwashirikisha wananchi katika maamuzi na uwekezaji wa miradi ya maendeleo

