*Wafikia Asilimia 90 katika utekelezaji wake
*Kukamilika Mwisho wa Mwezi Disemba 2026
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kupitia Mkoa wa KiTANESCO Kigamboni, limesema Mradi wa Kituo cha kupokea na kupoza umeme cha Dege umefikia asilimia 90.4 ya utekelezaji ukitarajia kukamilika Disemba 31,2026 ukiwa na lengo la kuimarisha hali ya upatikanaji wa umeme katika maeneo hayo na kuchochea shughuli za uzalishaji.
Akizungumza Novemba 18, 2026, baada ya kutembelea mradi huo, Meneja wa TANESCO Kigamboni, Mhandisi Godlove Mathayo, amesema kazi zinazoendelea kutekelezwa hivi sasa ni utekelezaji wa majaribio ya ndani ya mifumo ya kituo hicho pamoja na ujenzi wa njia sita mpya za kusambaza umeme ili kupunguza adha kwa wananchi ambao walikua wanapata umeme unaosafirishwa kutoka umbali mrefu.
Aidha, amesema tayari Transfoma mpya yenye uwezo wa MVA 120 imefungwa, ikiwa na uwezo mara mbili ya ile ya awali ya MVA 60. Hatua hiyo itaongeza uwezo wa kituo kukidhi mahitaji ya umeme yanayoendelea kuongezeka kutokana na shughuli za kiuchumi na kijamii katika eneo hilo.
Ameongeza kuwa upanuzi wa kituo hicho unaenda sambamba na ujenzi wa njia sita mpya za kusambaza umeme kwa wananchi, hatua itakayopunguza utegemezi wa njia moja ya awali yenye urefu wa zaidi ya kilomita 200, ambayo ilikuwa ikihudumia takribani asilimia 75 ya wananchi.
“Mradi huu una umuhimu mkubwa kwa wananchi wa Kigamboni. Kwa sasa baadhi ya wananchi wanakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa umeme kutokana na kuzimwa kwa muda kwa Kituo cha Dege ili kumpa Mkandarasi nafasi ya kufanya majaribio ya ndani ya mifumo pamoja na kazi za ujenzi wa njia sita mpya za usambazaji umeme. Hali hii inasababisha baadhi ya maeneo kukosa umeme kwa muda. Tunawaomba wananchi waendelee kuwa wavumilivu wakati kazi hizi zikiendelea, kwani mradi huu uko katika hatua za mwisho za utekelezaji,” amefafanua Mhandisi Mathayo.
Kwa upande wake, Mhandisi wa Mradi wa Dege, Edward Ngalamika, amesema Transfoma yenye uwezo wa MVA 120 iliwasili Oktoba 24, 2026, na kazi ya kuifunga imekamilika kwa asilimia 100.
Ameeleza kuwa utekelezaji wa mradi unaendelea vizuri, huku Mkandarasi akiendelea na hatua za majaribio ili kuhakikisha mifumo yote inafanya kazi kwa viwango vinavyotakiwa kabla ya kuanza kutumika kikamilifu.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi wa Kigamboni na maeneo jirani kwa kuimarisha upatikanaji wa umeme na kuchochea maendeleo ya shughuli za kiuchumi na kijamii.
Mradi wa Upanuzi wa Kituo cha Kupokea na Kupoza Umeme cha Dege, Kigamboni, ulianza kutekelezwa mwaka 2023 na unatarajiwa kukamilika Desemba 31, 2026. Mradi huo unatekelezwa na kampuni ya Telenerg Engineering LLC kutoka nchini Croatia.

