Akemea matumizi mabaya ya mamlaka kuwatisha wamiliki wa maeneo
▪ Ataka uwekezaji uwanufaishe pia wananchi wanaopisha miradi
WAZIRI MKUU, Dkt. Mwigulu Nchemba, amewataka maafisa wa ardhi kuzingatia sheria na kuhakikisha wananchi wanaopisha miradi ya maendeleo na uwekezaji wanalipwa fidia, akisisitiza kuwa matumizi ya maeneo hayo kwa manufaa ya umma hayapaswi kupuuza haki za wamiliki.
Amesema katika maeneo mbalimbali amekutana na malalamiko ya wananchi ambao mashamba yao yametumika kujenga shule, vituo vya afya na kutekeleza miradi mingine, lakini hawajalipwa fidia licha ya huduma kuanza kutolewa.
“Tuache kutumia vibaya sheria. Tuache kutumia vibaya mamlaka,” amesema.
Dkt. Mwigulu ameyasema hayo wakati akizungumza na wananchi katika viwanja vya Stendi ya Zamani ya Mailimoja, Kibaha, mkoani Pwani, baada ya kuzindua kitambulisho cha Taifa kilichoboreshwa.
Ameeleza kuwa Serikali inapohitaji ardhi kwa ajili ya miradi yenye maslahi mapana ya Taifa, wahusika wanapaswa kuzingatia masharti ya sheria na kulinda haki za wanaopisha maeneo hayo.
Amesema kuwepo kwa shule au kituo cha afya kinachotoa huduma hakuondoi wajibu wa kuzingatia haki ya mwananchi aliyekuwa akimiliki eneo hilo, likiwemo shamba la urithi wa familia.
Waziri Mkuu pia amekemea tabia ya baadhi ya maafisa kuwataka wananchi kurejesha hati zao kwa ahadi ya kupatiwa maeneo mengine, kisha maeneo hayo kuuzwa bila haki za wamiliki kuzingatiwa.
Amesisitiza kuwa wananchi wanapaswa kuunga mkono uwekezaji kwa sababu unaongeza ajira, uzalishaji na mapato ya nchi. Hata hivyo, amesema manufaa hayo yanapaswa kuwafikia pia wananchi wanaopisha miradi.
Dkt. Mwigulu amempongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kusimamia malipo ya fidia, akisema alipokuwa Waziri wa Fedha alishuhudia Serikali ikilipa madai ambayo baadhi yake yalikuwa yamedumu kwa miaka mingi.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu ameeleza kuwa Serikali imetanguliza malipo ya miradi ambayo wakandarasi walikuwa wamesimamisha kazi, ikifuatiwa na malipo ya awali kwa miradi yenye mikataba, kabla ya kusaini mikataba mipya iliyokamilisha taratibu za manunuzi.
Amewataka wakandarasi waliopokea fedha kurejea kazini na kuongeza kasi ya utekelezaji ili wananchi wapate huduma zilizokusudiwa.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Dkt. Pius Stephen Chaya, amesema Serikali imeandaa utaratibu wa kulipa kwa awamu wananchi wanaodai fidia katika eneo maalumu la uwekezaji la Bagamoyo.
Amesema hatua hiyo inafuatia maelekezo ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha wananchi hao wanalipwa.
Naye Waziri wa Maji, Juma Aweso, ameelekeza madai ya mkandarasi wa mradi wa maji Pangani ya shilingi milioni 700 yalipwe kabla ya mwezi huu kuisha ili kuharakisha utekelezaji.
Pia, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) kuanza utaratibu wa kuwapatia wananchi wa Pangani maji bila kusubiri ujenzi wa tenki ukamilike.