Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ameshiriki katika Mkutano wa Majadiliano ya Viongozi kuhusu Uwekezaji katika Miundombinu kati ya Afrika na Singapore, uliofanyika Singapore tarehe 17 Novemba 2026.
Mkutano huo, ulioandaliwa kwa ushirikiano na Invest Africa, Connect Africa Southeast Asia na Taasisi ya Maendeleo ya Miundombinu Binafsi (Private Infrastructure Development Group – PIDG), uliwakutanisha mawaziri, wawekezaji na viongozi wa fedha na Mawasiliano. Mkutano huo uliendeleza mkutano wa Viongozi kujadiki kuhusu “Kugharamia Mustakabali wa Kidijitali wa Tanzania” uliofanyika London tarehe 8 Oktoba 2026, sambamba na Jukwaa la Uwekezaji la Tanzania.
Katika hotuba yake pamoja na mambo mengine, Waziri Kairuki aliwakaribisha wadau kuungana na Tanzania katika kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwa gharama nafuu na kuimarisha nafasi ya Nchi kama kitovu cha kikanda cha huduma za kidijitali. Alieleza kuwa azma hii imejikita katika Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 na Mpango Mkakati wa Uchumi wa Kidijitali wa Mwaka 2024–2034, chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Waziri Kairuki alieleza misingi ambayo tayari imewekwa ikiwemo Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano wenye urefu wa zaidi ya kilomita 15,000, ambao umeshafikishwa katika mikoa yote na wilaya 122 kati ya 139 za Tanzania Bara ambayo Wilaya zilizosalia zotakuwa zomeshaunganishea ifikapo Mwezi Desemba 2026. Alielezea pia mpango wa kuuunganisha na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ifikapo Aprili 2027. Alisisitia pia kwamba tayari huduma ya 4G inawafikia zaidi ya wananchi asilimia 94 , na kwa upande wa 5G takriban asilimia 34 wamefikiwa.
Mhe. Kairuki aliwasilisha maeneo 5 ya kipaumbele kwa uwekezaji katika Miundo mbinu ya Kidijitali:
(i)Muunganisho wa mkongo wa kikanda na uwezo wa jumla (wholesale capacity);
(ii) Vituo vya kuhifadhi data na huduma za wingu (cloud), ikiwemo Dodoma na Zanzibar;
(iii) Muunganisho wa maeneo ya mwisho (last-mile) na vijijini;
( iv) 5G na mitandao ya kisasa; na
( v) Miundombinu ya umma ya kidijitali kwa ajili ya utambulisho, malipo na ubadilishanaji wa taarifa.
Waziri Kairuki alieleza kuwa Tanzania iko tayari kwa fursa za uwekezaji wa pamoja katika Miundombinu ya Kidijitali.
“Tunawakaribisha kufanya kazi nasi nchini Tanzania ili kuigeuza Dira 2050 kuwa miradi yenye tija kibiashara na manufaa ya kudumu kwa umma,” alisema Mhe. Kairuki.
Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari itaendelea kushirikiana na wawekezaji na Wadau wa maendeleo ili kugeuza vipaumbele hivi kuwa miradi inayotekelezeka kwa manufaa ya Watanzania wote.

