Na Sixmund Begashe, Ngorongoro

TANZANIA imepongezwa kwa kazi nzuri ya uhifadhi endelevu wa Hifadhi ya Eneo la Mamlaka ya Ngorongoro hatua inayowavutia watu wengi kutembelea eneo hilo. 

Pongezi hizo zimetolewa na Wajumbe wa Mkutano wa 24 wa Jukwaa Uhifadhi wa Wanyamapori Barani Afrika (24th African Wildlife Consultanive Forum) walipotembelea eneo hilo lenye mvuto wa kipekee Duniani.

Bw. Eardley Rudman kutoka Afrika Kusini amesema kuwa, amejiona wa bahati kubwa kutembelea Ngorongo eneo lililohifadhiwa vyema. 

Ameongeza kuwa kutokana na utajiri mkubwa wa vivutio alivyoshuhudia inamsukuma kupanga safari nyingine ya kulitembelea eneo hilo. 

Pamoja na kuipongeza Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kuandaa safari hiyo ya kitalii, Bi. Sylvia Van Staden kutoka nchini Zambia, amesema wametumia muda mfupi ndani ya eneo hilo, lakini wameweza kuwaona wanyama wote wakubwa na mandhari ya kuvuta zaidi.  

Naye Afisa Wanyamapori Mkuu Idara ya Wanyamapori katika Wizara ya Maliasili na Utalii Frederick Ligate, amesema lengo la safari hiyo ya utalii ni sehemu ya kuunga mkono juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuutangaza utalii Kitaifa na Kimataifa. 

Ameongeza kuwa, wajumbe hao ni wadau wakubwa wa utalii Barani Afrika hivyo baada ya kujionea utajiri wa vivutio nchini watahamasika kuwa mabalozi wazuri wa utalii wa Tanzania katika nchi zao.