MBUNGE wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania, Cosato Chumi, amezitaka nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuimarisha mshikamano na ushirikiano wa kikanda kwa kuongeza biashara baina yao ili kukabiliana na athari za migogoro ya kimataifa.

Chumi amesema migogoro inayoendelea katika maeneo mbalimbali duniani imeonesha umuhimu wa nchi za Afrika Mashariki kujenga uchumi imara unaoweza kukabiliana na misukosuko ya kimataifa, hususan katika sekta za nishati, kilimo, mbolea na biashara.

Akizungumza katika semina ya mahusiano ya mabunge kati ya Bunge la Afrika Mashariki na Bunge la Umoja wa Ulaya (Interparliamentary Relations Seminar), amesema Jumuiya hiyo yenye soko la zaidi ya watu milioni 300 ina fursa kubwa ya kujenga nguvu ya kiuchumi kupitia biashara ya ndani ya kikanda.

Amesema hatua muhimu zinazopaswa kupewa kipaumbele ni kuondoa vikwazo vya kibiashara kati ya nchi wanachama, kuimarisha uzalishaji wa ndani na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa katika ukanda huo ili kupunguza utegemezi wa masoko na nguvu za kiuchumi kutoka nje.

Aidha, amesisitiza kuwa Bunge la Afrika Mashariki (EALA), kwa kushirikiana na mabunge ya kitaifa, lina jukumu muhimu la kuweka na kusimamia sheria pamoja na mifumo inayolinda amani, usalama na ustawi wa kiuchumi wa wananchi.

Chumi amesema ushirikiano wa kikanda haupaswi kuchukuliwa kama jambo la hiari, bali ni hitaji la kimkakati katika kuhakikisha usalama wa kiuchumi, kuharakisha maendeleo na kuboresha maisha ya wananchi wa Afrika Mashariki.

Semina hiyo imejadili athari za migogoro ya kimataifa na mabadiliko ya mifumo ya biashara duniani, pamoja na mikakati ambayo mabunge yanaweza kutumia kulinda usalama wa kiuchumi na kuimarisha ushirikiano wa kikanda.

Katika majadiliano hayo, imeelezwa kuwa migogoro ya kimataifa ni fundisho kwa nchi za Afrika Mashariki kuhusu umuhimu wa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani na kujenga mifumo ya kiuchumi inayoweza kustahimili changamoto zinazotokana na mabadiliko ya hali ya kisiasa na kiuchumi duniani.