Na Mwandishi Wetu- Morogoro.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera Bunge Uratibu na Wenye Ulemavu) Dkt, Jim Yonazi amehimiza watendaji wa serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya kitaasisi ya Ufuatiliaji na tathimini sambamba na ushirikiano wa kazi katika hatua za mipango ya bajeti.

Kauli Hiyo ameitoa Mkoani Morogoro leo tarehe 17/11/2026 wakati akifungua mafunzo ya kimkakati ya uongozi katika ufuatiliaji na tathimini yaliyohusisha Wakurugenzi wa Ufuatiliaji na Tathimini, Wakurugenzi wa Mipango wa wizara, Wakurugenzi kutoka Serikali za Mikoa.

Ameongeza kusema hatua hiyo itasaidia katika kuimarisha kutambua mahitajia ya tathimini na kusimamia tathimini zinajibu maswali muhimu katika utekelezaji wa shughuli za serikali, ikiwa ni pamoja na kuimarisha mawasiliano yenye Ushahidi kwa ajili ya kufanya maamuzi ya kimkakati wa viongozi wetu.

“Maamuzi ambayo yataleta mabadiliko na kuharakisha mafanikio kwa wananchi wetu huku tukizingatia uimarishwaji wa matumizi ya tehama na kuzingatia umuhimu wa kujifunza uwajibikaji na kuchukua hatua kuboresha utendaji,”alieleza Dkt, Yonazi.  

Aidha, ni muhimu kuwa na mawazo ya kujifunza ili kuhakikisha maarifa tunayoyapata yanatutoa kutoka hatua moja kwenda nyingine, maarifa hayo lazima yatumike ipasavyo ili yalete maana zaidi kwa jamii.

Awali, Mkurugenzi wa Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bi. Sakina Mwinyimkuu, amesema kuwa mafunzo hayo kwa viongozi ni muhimu katika kuimarisha usimamizi wa shughuli za Ufuatiliaji na Tathmini, hususan katika kipindi hiki ambacho Serikali inaendelea na utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

“mafunzo haya, yanatarajiwa kuendelea kufanyika kila mwaka, ili kuendelea kuleta mabadiliko chanya katika usimamizi wa mipango, ufuatiliaji wa utekelezaji wake pamoja na tathmini ya matokeo, katika kuongeza ufanisi na utekelezaji wa mipango ya maendeleo kwa ujumla,” alieleza.

Bi. Mwinyimkuu ameishukuru Taasisi ya Uongozi kwa kuratibu mafunzo hayo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, akieleza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kuimarisha uwezo wa viongozi na wataalamu katika eneo la Ufuatiliaji na Tathmini. 

Kwa upande Bw, Gerald Peter Sondo Mkuu wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathimini Jiji la Dar es Salaam, amesema kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha ushirikiano na unganishaji wa sekta kupitia matumizi ya takwimu na ushahidi katika kupanga na kutekeleza mipango ya maendeleo.

“Mafunzo yametuwezesha washiriki kujikita katika matumizi ya ufanisi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwemo matumizi ya Akili Unde (AI) katika kuchambua, kuandaa na kuchakata taarifa mbalimbali kwa weledi na kwa muda mfupi,” alibainisha.

Bw, Sondo amehimiza kuongeza umakini kwa taarifa zinazozalishwa au kuchakatwa kwa kutumia AI kwa kufanya uhakiki wa kina kabla ya kutolewa kwa umma.