Tanzania imesisitiza dhamira yake ya kuendelea kuunga mkono juhudi za Umoja wa Afrika (AU) katika kukuza amani, usalama na utulivu barani Afrika, kwa kuimarisha taasisi za kikanda na mshikamano miongoni mwa nchi wanachama.

Dhamira hiyo imesisitizwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, wakati akitoa hotuba ya ukaribisho katika Mkutano wa 18 wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika (PSC), unaofanyika jijini Arusha tarehe 16 na 17 Novemba 2026.

Balozi Shelukindo amesema maamuzi yanayofikiwa na Baraza hilo yanapaswa kuambatana na hatua madhubuti za utekelezaji ili kuhakikisha yanazaa matokeo chanya kwa wananchi na kusaidia kupata suluhu za kudumu za migogoro inayolikabili bara la Afrika.

Aidha, Balozi Shelukindo alitumia fursa hiyo kuwaalika wajumbe wa mkutano huo kurejea nchini Tanzania mwaka 2027 kuhudhuria mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), yatakayoandaliwa kwa pamoja na Tanzania, Uganda na Kenya. Vilevile, aliwaalika kushiriki mashindano ya Miss World 2027, ambayo pia Tanzania itakuwa mwenyeji.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza hilo kwa mwezi Novemba 2026 ambaye pia ni Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Côte d’Ivoire katika Umoja wa Afrika, Mhe. Balozi Antonin B. Bieke, amesema mapitio ya mbinu za kazi za Baraza yanapaswa kuongeza ufanisi katika kukabiliana na changamoto za amani na usalama barani Afrika, zikiwemo ugaidi, mabadiliko ya tabianchi, uhalifu wa kupangwa unaovuka mipaka na vitisho vya kimtandao.

Akizungumza katika mkutano huo, Kamishna wa Umoja wa Afrika anayeshughulikia Masuala ya Siasa, Amani na Usalama, Mhe. Balozi Bankole Adeoye, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha uwezo wa Baraza katika kutekeleza majukumu yake, kutathmini mafanikio na kuweka mapendekezo ya vitendo yatakayoboresha utendaji wake.

Mkutano huo wa siku mbili, unaofanyika chini ya uenyekiti wa Jamhuri ya Côte d’Ivoire, unawakutanisha wajumbe wa Baraza na wawakilishi wa Tume ya Umoja wa Afrika kwa lengo la kupitia mbinu za kazi za Baraza na kuweka mikakati ya kuimarisha amani na usalama barani Afrika.