Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha

………….

Na  Happy Lazaro

Mrajis Msaidizi wa Ushirika Mkoa wa Dodoma, Joseph Chitinka, amewahimiza watumishi wa umma kujiunga na vyama vya ushirika vya kuweka na kukopa (SACCOs), akieleza kuwa vyama hivyo ni nyenzo muhimu katika kuwawezesha kiuchumi kupitia uwekaji wa akiba na upatikanaji wa mikopo yenye masharti yanayozingatia taratibu.

Ameyasema hayo leo jijini Arusha wakati akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 23 wa PCCB SACCOS wa mwaka 2026 unaofanyika mkoani Arusha.

Chitinka amesema SACCOs zinatoa fursa kwa wanachama kuweka fedha zao na kukopa kulingana na uwezo wao, huku zikiwa na mifumo inayosimamia shughuli za kifedha kwa kuzingatia sheria na kanuni za ushirika.

Ameeleza kuwa vyama hivyo ni sehemu salama ya kupata mikopo ikilinganishwa na baadhi ya taasisi nyingine za kifedha ambazo hutoza riba kubwa na wakati mwingine kuwaweka wakopaji katika mazingira magumu ya kurejesha madeni.

Chitinka amesema ni muhimu kwa watumishi ambao bado hawajajiunga na vyama vya ushirika kutumia fursa hiyo, huku akiwataka viongozi wa SACCOs kuongeza juhudi za kuwafikia na kuwahamasisha watumishi hao ili kuongeza idadi ya wanachama.

Aidha, amesisitiza kuwa SACCOs ni mali ya wanachama wenyewe, hivyo wanapaswa kushiriki kikamilifu katika maamuzi na usimamizi wa vyama vyao ili kuhakikisha vinaendeshwa kwa uwazi, uwajibikaji na kwa manufaa ya wote.

Chitinka amewataka wanachama kuzingatia nidhamu ya urejeshaji wa mikopo kwa wakati, akieleza kuwa tabia hiyo itasaidia kupunguza mikopo chechefu na kuongeza uwezo wa vyama kuendelea kutoa huduma za mikopo kwa wanachama wengine.

Ameongeza kuwa urejeshaji mzuri wa mikopo una mchango mkubwa katika kukuza mtaji wa vyama, kuongeza faida na kuimarisha mshikamano miongoni mwa wanachama, ambao ndio msingi wa mafanikio ya vyama vya ushirika.

“Ushirikiano kati ya wanachama, viongozi na wasimamizi wa vyama hivyo ni muhimu katika kuhakikisha SACCOs zinaendelea kuwa imara, zinakuwa na uwezo wa kifedha na zinatimiza lengo la kuwawezesha wanachama kiuchumi.”amesema Chintika.