
Na Mwandishi wetu, Babati
NAIBU Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Regina Ndege amewapatia watu wenye uhitaji maalum Mkoani Manyara viti mwendo 50, fimbo nyeupe 20 magongo 20 kwa watu wenye changamoto ya kutembea na kofia, miwani na mafuta kwa watu 35 wenye ulemavu wa ngozi.
Naibu Waziri Regina ambaye pia ni Mbunge wa viti maalum wa Mkoa wa Manyara, ametoa msaada huo Mjini Babati kwenye hafla ya chakula cha pamoja na ugawaji wa vifaa maalum kwa watu wenye uhitaji maalum.
Amewataka wahitaji hao waliopatiwa vifaa hivyo mbalimbali kuvitunza ili viweze kuwasaidia katika maisha yao ya kila siku tofauti na kabla hawajavipata.
Ametaja vifaa hivyo alivyotoa ni viti mwendo 50, fimbo nyeupe 20 kwa watu wenye matatizo ya macho na magongo 20 kwa watu wenye changamoto ya kutembea.
“Pia tumetoa kwa watu 35 wenye matatizo ya ulemavu wa ngozi kwa kuwapatia kofia, miwani na mafuta ya kukinga ngozi zao wakati wa jua,” amesema Naibu Waziri Regina.
Mmoja kati ya wanufaika hao, Magdalena John amemshukuru Naibu Waziri Regina kwa kumsaidia kiti mwendo kwani kwa muda mrefu alikuwa amekaa ndani ya nyumba kwa kushindwa kutembea.
“Namshukuru sana Naibu Waziri kwani viti mwendo vimetusaidia mno na kwa miaka miwili sikuweza kutembea kutokana na miguu na mifupa kuuma na leo Naibu Waziri Regina ameninyanyua kwa kutumia kiti mwendo,” amesema Magdalena.
Kiongozi wa madhehebu ya kiislamu Shafii Shaban amesema matendo ya huruma ya kuwasaidia watu wenye uhitaji yanapaswa kuigwa kwani Naibu Waziri Regina amekuwa mfano,
“Siyo kwamba hawa wametatuliwa shida zao zote hapana tumeona tuu moyo wa upendo kwa watu wenye ulemavu ulionyeshwa na Naibu Waziri Regina ni wa kuigwa,” amesema Shaban.
Mdau wa watu wenye ulemavu, Letion Lucas amewaomba viongozi wengine na jamii kwa ujumla kuiga mfano wa Naibu Waziri Regina kwa kuwajali wengine hasa watu wenye mahitaji maalum.
Letion amesema katika eneo lenye baraka ni pamoja na kuwajali wale wenye uhitaji maalum waliosahaulika, kwani hawawezi kutafuta wenyewe, inakuwa faraja kwao wanaona hawajatengwa wala kusahaulika.
