Paris, 16 Novemba 2026,
Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Saidi Othman Yakubu, leo amekutana na kufanya mazungumzo na Mhe. Louise Morel, Mbunge wa Jimbo la Sita la Bas-Rhin na Mwenyekiti wa Kundi la Urafiki wa Kibunge kati ya Ufaransa na Tanzania, kuhusu kuimarisha ushirikiano katika utalii, uwekezaji na mahusiano baina ya mabunge.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Morel ameeleza kuwa kundi analoliongoza lina wabunge 20 marafiki wa Tanzania, likiwa jukwaa muhimu la kuendeleza uhusiano na kupanua ushirikiano wenye manufaa kwa wananchi wa nchi zote mbili.
Viongozi hao wamejadili namna ya kutumia jukwaa hilo kutangaza vivutio vya utalii vya Tanzania nchini Ufaransa, kuhamasisha uwekezaji na kuimarisha mahusiano kati ya wabunge wa nchi hizo.
Balozi Yakubu pia amewasilisha salamu za Mheshimiwa Spika Mussa Azzan Zungu,(Mb) wa Bunge la Tanzania, ambaye alimweleza kuwa alikutana na wabunge wa Ufaransa katika mkutano wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU) uliofanyika hivi karibuni jijini Arusha.
Aidha, Balozi Yakubu amemweleza Mhe. Morel kuwa Tanzania iko tayari kuunda Kundi la Urafiki wa Kibunge na Ufaransa katika Bunge lake, ili kuimarisha mawasiliano na ushirikiano wa moja kwa moja kati ya mabunge hayo kwa manufaa ya pande zote mbili.
Mazungumzo hayo yameangazia nafasi ya diplomasia ya kibunge katika kuimarisha urafiki wa Tanzania na Ufaransa na kuufungamanisha na fursa za kiuchumi, hususan katika sekta za utalii na uwekezaji.
