Na OWM (KAM), Dar es Salaam
Naibu Waziri , Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Dkt. Evaline Munisi, amesema Serikali inaendelea kuimarisha mazingira ya ajira na kutoa mafunzo ya ujuzi yanayowezesha vijana na wanawake kujiajiri kupitia sekta mbalimbali za kiuchumi.
Akizungumza Novemba 14, 2026 katika Kongamano la wanawake na wanaume wajariamali na uzinduzi wa mpango wa “Jiko Lako, Fursa Yako,” Dkt. Munisi amesema sekta ya upishi ina mnyororo mpana wa shughuli za kiuchumi unaohusisha kilimo, ufugaji, usindikaji, usafirishaji na huduma za chakula, ambazo zina uwezo wa kuzalisha ajira na kuongeza kipato kwa wananchi.
Amesema, Serikali inaendelea kuwawezesha vijana na wanawake kupata mafunzo ya ufundi stadi na ujasiriamali kupitia programu ya Taifa ya Kukuza Ujuzi ili kuwaandaa kukabiliana na mahitaji ya soko la ajira. Pia, imeendelea kuweka mazingira ya upatikanaji wa mitaji kupitia mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri pamoja na Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Aidha, amewataka wamiliki wa biashara za upishi kuzingatia sheria za kazi kwa kuhakikisha wafanyakazi wanapata mikataba ya ajira, malipo stahiki na mazingira salama ya kufanyia kazi, akisisitiza kuwa ukuaji wa biashara unapaswa kwenda sambamba na ustawi na haki za wafanyakazi.
Dkt. Munisi amewahimiza vijana na wanawake kutumia mpango huo kuanzisha na kukuza biashara za upishi, akibainisha kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta hiyo ili kuwezesha upatikanaji wa ujuzi na fursa za kiuchumi.
“Jiko linaweza kuwa kitega uchumi chenye uwezo wa kuzalisha ajira na kuchangia maendeleo ya wananchi,” amesema
Naye, Muandaaji wa kipindi cha Masotojo Jacqueline Salon, ameishukuru Serikali kwa kuungana nao katika shughuli hiyo, akisema ushirikiano huo ni chachu ya kuhamasisha jamii kutambua fursa zilizopo katika sekta ya upishi na kukuza shughuli za ujasiriamali, hususan kwa vijana na wanawake.
Kwa upande wake, Bi Mariam Juma Mmoja wa washiriki wa kongamano hilo, ameiomba Serikali kuendelea kuandaa majukwaa ya aina hiyo yanayowaunganisha wajasiriamali na wadau mbalimbali ili kuwapatia fursa za kujifunza, kubadilishana uzoefu na kutafuta masoko ya bidhaa na huduma zao. Amesema kongamano hilo limekuwa fursa muhimu kwa wanawake kujifunza namna ya kutumia ujuzi wa upishi kujiajiri, kukuza biashara zao na kuongeza kipato.

