Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akizungumza wakati wa hafla ya uwekaji wa mawe ya msingi ya miradi ya elimu Mtopepo na Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), leo tarehe 16 Novemba 2026, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa karakana za kisasa za uhandisi katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), leo tarehe 16 Novemba 2026, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, akiweka jiwe la msingi la ujenzi wa Skuli ya Msingi Mtopepo, leo tarehe 16 Novemba 2026, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.

Muonekano wa jengo jipya la Skuli ya Msingi Mtopepo lililowekwa jiwe la msingi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, leo tarehe 16 Novemba 2026, Mtopepo, Mkoa wa Mjini Magharibi, Zanzibar.
……………
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, amesema Serikali ya Awamu ya Nane itaendelea kuwekeza katika sekta ya elimu kwa kujenga na kuboresha miundombinu ya skuli, pamoja na kuimarisha elimu ya ufundi na mafunzo ya amali, ili wananchi wapate elimu bora na vijana wawe na ujuzi unaokidhi mahitaji ya soko la ajira na uchumi wa kisasa.
Rais Dkt. Mwinyi ameyasema hayo leo, tarehe 16 Novemba 2026, katika hafla za uwekaji wa mawe ya msingi ya ujenzi wa Skuli ya Msingi Mtopepo na karakana za kisasa za uhandisi katika Taasisi ya Karume ya Sayansi na Teknolojia (KIST), Mkoa wa Mjini Magharibi.
Amesema Serikali imejielekeza kuhakikisha mipango na ahadi ilizotoa kwa wananchi zinatafsiriwa kwa vitendo na kuleta matokeo yanayoonekana katika kuboresha maisha yao, hususan katika sekta muhimu za huduma za kijamii.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali inatambua ongezeko la idadi ya watu na mahitaji makubwa ya huduma za elimu, hususan Mkoa wa Mjini Magharibi ambao, kwa mujibu wa Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2022, una wakazi 893,169, sawa na asilimia 47.3 ya wakazi wote wa Zanzibar.
Ameeleza kuwa hali hiyo imeongeza mahitaji ya madarasa, walimu na miundombinu mingine ya kufundishia na kujifunzia, hivyo Serikali inaendelea kujenga skuli mpya na kuongeza madarasa ili kupunguza msongamano wa wanafunzi na kuboresha mazingira ya elimu.
Aidha, amesema Serikali imejielekeza kujenga skuli za kisasa zinazokidhi mahitaji ya elimu ya sayansi na teknolojia, zikiwa na maabara, miundombinu ya TEHAMA pamoja na mazingira rafiki na salama kwa wanafunzi wote, wakiwemo wenye mahitaji maalumu.
Amesema uwekezaji huo unaenda sambamba na mageuzi ya mitaala ya elimu ya maandalizi na msingi yaliyoanza mwaka 2023, yanayolenga kuwajengea wanafunzi maarifa, stadi na umahiri wa kukabiliana na changamoto za kielimu.
Dkt. Mwinyi amesema Serikali imeanza ujenzi wa skuli nyingine katika eneo la Mtopepo yenye ghorofa nne, madarasa 50 na lifti, hatua itakayosaidia kupunguza changamoto ya msongamano wa wanafunzi katika madarasa.
Amesema ujenzi wa skuli za ghorofa nne zenye lifti ni hatua mpya katika historia ya Zanzibar, inayolenga kutumia ardhi kwa ufanisi na kuongeza nafasi za utoaji wa huduma za elimu. Miradi ya aina hiyo pia inatekelezwa katika maeneo ya Kinuni, Bububu, Kwerekwe B, Kwamtipura, Mwambe na Shamiani.
Akizungumzia ujenzi wa karakana nne za kisasa KIST, Rais Dkt. Mwinyi amesema Serikali inalenga kuimarisha taasisi hiyo katika kuandaa wataalamu wenye ujuzi wa sayansi, teknolojia na uhandisi, ili kuunga mkono azma ya kujenga uchumi wa kisasa na wenye ushindani kama ilivyoainishwa katika Dira ya Maendeleo ya Zanzibar 2050.
Amesema karakana hizo zitahusisha fani za Uhandisi wa Ujenzi, Uhandisi wa Mitambo, Useremala na Ufundi wa Magari, na kuongeza uwezo wa taasisi hiyo kutoa mafunzo ya vitendo yanayowaandaa vijana kwa mahitaji ya soko la ajira.
Aidha, amesema Serikali inaendelea kupanua wigo wa elimu ya ufundi na mafunzo ya amali kwa kujenga vyuo Bweleo, Unguja na Chambani, Pemba, sambamba na kuimarisha mafunzo ya ubaharia kupitia ujenzi wa Taasisi ya Mafunzo ya Bahari.
Rais Dkt. Mwinyi amewataka wakandarasi na wasimamizi wa miradi hiyo kuhakikisha kazi zinakamilishwa kwa wakati na kwa kuzingatia viwango vya ubora vilivyowekwa, huku akisisitiza umuhimu wa uzalendo, uadilifu na uwajibikaji katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.
Pia amewaomba wananchi wanaoishi katika maeneo yanayozunguka miradi hiyo kuendelea kutoa ushirikiano kwa wakandarasi na wasimamizi ili kuwezesha kazi kukamilika kwa ufanisi.
Kwa upande wake, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Mhe. Lela Mohammed Mussa, amesema ujenzi wa skuli za kisasa zenye miundombinu bora utaimarisha mazingira ya kufundishia na kujifunzia na kusaidia kuongeza kiwango cha ufaulu wa wanafunzi.
Katika hafla hiyo, Rais Dkt. Mwinyi ameishukuru Taasisi ya Zayed pamoja na Ubalozi wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu na kuchangia uwekezaji unaolenga kuboresha mustakabali wa watoto wa Zanzibar.
