
Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, akizungumza na waandishi wa habari kando ya mkutano waWorld Diet Initiative, uliowakutanisha wadau Kutoka nchi zaidi ya 16 kwa lengo la kuchunguza na kuhifadhi vyakula vya asili vinavyotumiwa na jamii mbalimbali duniani, uliofanyika leo Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dar es Salaam
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Katika juhudi za kukabiliana na changamoto ya utapiamlo na magonjwa yasiyoambukiza duniani, wadau wa masuala ya lishe kutoka nchi 15 wamekutana katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kujadili mikakati ya kuimarisha matumizi ya vyakula vya asili kwa ajili ya kuboresha afya za jamii.
Wadau wametoka mataifa mbalimbali ya Afrika, Asia, Ulaya na Amerika Kusini, ikiwemo Tanzania na Uganda, wamekutana katika kongamano la siku mbili lililoandaliwa na MUHAS kwa lengo la kubadilishana uzoefu, kujadili matokeo ya tafiti za kisayansi na kuweka mikakati ya kuhamasisha jamii kutumia vyakula vinavyopatikana katika mazingira rafiki.
Akizungumza Novemba 16, 2026, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa kongamano hilo, Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Bruno Sunguya, amesema changamoto ya lishe bado inaendelea kuzikabili Tanzania na mataifa mengine yanayoendelea, kutokana na mabadiliko ya mifumo ya ulaji, ikiwemo kuongezeka kwa matumizi ya vyakula vilivyosindikwa.
Profesa Sunguya amesema vyakula vingi vya viwandani vina kiwango kikubwa cha mafuta, sukari na viambata vingine vinavyoweza kuathiri afya ya binadamu vinapotumiwa kupita kiasi, hivyo kuna umuhimu wa kurejea katika matumizi sahihi ya vyakula vya asili vinavyopatikana nchini.
“Tanzania ni sehemu ya mpango huu, na Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili kimekuwa mstari wa mbele katika jitihada za kupambana na changamoto ya lishe. Changamoto hii inaweza kutatuliwa iwapo tutatumia vyakula vya asili vilivyopo kwa namna inayofaa,” amesema Profesa Sunguya.
“Jitihada hizi zinaangalia namna ya kuongeza thamani ya vyakula vya asili kupitia tafiti za kisayansi, ili kubaini manufaa yake kiafya na kuhakikisha vinahifadhiwa vizuri. Ni muhimu matokeo hayo yakawafikia wananchi na kuwahamasisha kuvitumia katika maisha yao ya kila siku,” amesisitiza.
Naibu Makamu Mkuu wa Chuo cha MUHAS, Profesa Sabina Mugusi, amesema taasisi hiyo ina programu zinazolenga kushughulikia changamoto za lishe na magonjwa yasiyoambukiza kupitia tafiti na machapisho mbalimbali ya kitaalamu.
Amesema matokeo ya tafiti hizo yameonesha umuhimu wa lishe inayotokana na vyakula vya asili katika kuzuia magonjwa sugu yasiyoambukiza, hatua iliyochangia kuanzishwa kwa mpango wa lishe duniani uliozinduliwa katika kongamano hilo.
Akifafanua kuhusu tafiti hizo, Dkt. Temba amesema utafiti wa awali ulifanyika katika Mkoa wa Kilimanjaro kwa kuhusisha vyakula vya asili vinavyopatikana katika eneo hilo, huku akibainisha kuwa kuna uwezekano wa matokeo yake kutoa mwanga katika tafiti zitakazofanyika maeneo mengine nchini kutokana na kufanana kwa baadhi ya mifumo ya vyakula vya asili.
Amesema kukutana kwa wadau hao kutoka mataifa mbalimbali kutasaidia kupanua wigo wa tafiti, kubadilishana maarifa na kuimarisha matumizi ya ushahidi wa kisayansi katika kutatua changamoto za lishe, huku akieleza kuwa mpango huo unalenga kuhakikisha vyakula vya asili vinapata nafasi kubwa katika mikakati ya kuboresha afya ya jamii duniani.
