NA DENIS MLOWE, IRINGA
WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Dkt. Joel Arthur Nanauka, amewataka vijana nchini kutumia fursa zinazotolewa na Serikali kujiajiri, kuanzisha biashara na kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo ya taifa badala ya kusubiri kuajiriwa.
Akizungumza na wanavyuo kutoka vyuo vikuu mbalimbali vya Mkoa wa Iringa katika jukwaa la Campus Connect lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Mkwawa, Nanauka alisema Serikali imeendelea kuweka mazingira yanayowawezesha vijana kuwa sehemu muhimu ya maamuzi ya kitaifa, kisiasa, kiuchumi na kisera.
Alisema ushiriki wa vijana katika michakato ya maamuzi umeanza kuleta matokeo akibainisha kuwa Serikali imeendelea kuimarisha sera na mifumo inayolenga kuongeza fursa za kiuchumi kwa kundi hilo.
Alitaja hatua mojawapo kuwa ni maboresho ya sheria na mifumo ya manunuzi ya umma, ambapo amesema asilimia 30 ya manunuzi ya umma inaelekezwa kwa makundi maalumu yakiwemo vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu ili kuwawezesha kushiriki katika zabuni za Serikali.
Alizitaja baadhi ya huduma ambazo vijana wanaweza kuzifanya kupitia kampuni zao kuwa ni usafi wa ofisi na taasisi za Serikali usambazaji wa vifaa vya maandishi, huduma za chakula na vinywaji, pamoja na shughuli za utangazaji na utengenezaji wa nembo za taasisi.
Alisema vijana wanapaswa kuacha dhana kwamba ajira pekee ni kuajiriwa serikalini au katika kampuni kubwa, badala yake watambue kuwa wanaweza kuanzisha biashara ndogo na kuzikuza hatua kwa hatua.
Aidha, aliwataka wanafunzi kutambua kuwa elimu ya chuo kikuu haipaswi kuwa maandalizi ya kutafuta ajira pekee bali ni sehemu ya kujenga uwezo, ubunifu, mahusiano ya kimkakati na maarifa yatakayowawezesha kukabiliana na changamoto za maisha.
Alisema neno chuo kikuu linahusisha maarifa mapana yanayopaswa kumwezesha mhitimu kufanya kazi katika mazingira mbalimbali duniani, hivyo wanafunzi wanapaswa kutumia muda wao chuoni kujenga uwezo unaozidi maarifa wanayopata darasani.
Nanauka alisisitiza umuhimu wa kujenga mtandao wa watu wenye uwezo na fursa mbalimbali, akieleza kuwa mahusiano ya kimkakati yanaweza kuwa nyenzo muhimu katika kufungua milango ya mafanikio katika maisha ya kijana.
Alisema mafanikio ya mtu hayapimwi kwa aina ya kazi anayofanya, bali namna anavyoifanya kazi hiyo kwa ubora, kujituma na kuithamini.
Alitoa wito kwa vijana kuheshimu kila aina ya kazi na kuitumia kama fursa ya kujifunza, kupata uzoefu na kujijengea uwezo wa kufanya mambo makubwa zaidi.
Akizungumzia changamoto za kifikra, Nanauka alisema baadhi ya vijana wamekuwa wakikwamishwa na imani hasi kuhusu uwezo wao, hali inayoweza kuwafanya washindwe kutumia fursa zilizopo mbele yao.
Aliwataka kuanza kujenga mtazamo chanya kuhusu maisha yao, kujiamini na kuondoa fikra zinazowafanya wajione hawawezi kufikia malengo yao.
Alisisitiza kuwa kila kijana anapaswa kuwa na ndoto, kuweka malengo na kuchukua hatua za kuyafikia, akieleza kuwa mazingira ya mtu aliyotoka hayawezi kuwa kipimo cha mwisho cha mafanikio yake.

